Shirika la Posta Tanzania (TPC) kupitia Ofisi yake ya Mkoa wa Mbeya, limeadhimisha Wiki ya Posta Duniani kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kukabidhi msaada wa vyandarua katika Hospitali ya Wilaya ya Igawilo, Jijini Mbeya.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Mbeya, Amos Millinga, alisema kuwa wiki hiyo imelenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali za Posta, sambamba na kuadhimisha Siku ya Posta Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Oktoba.
“Wiki hii tumeendesha programu maalum inayolenga kutoa uelewa wa huduma zetu za Posta. Lakini sambamba na hilo, tunasherehekea Siku ya Posta Duniani kwa kujihusisha na shughuli za kijamii kama njia ya kurudisha fadhila kwa jamii,” alisema Millinga.
Millinga aliongeza kuwa Shirika la Posta ni miongoni mwa mashirika ya umma yanayojali ustawi wa jamii, na kila mwaka limekuwa likitenga sehemu ya bajeti yake kusaidia sekta za afya, elimu na mazingira.
“Tumeamua kufika hapa Hospitali ya Igawilo kukabidhi vyandarua ambavyo vitasaidia wagonjwa na wadau mbalimbali wanaopokea huduma katika hospitali hii. Tunafanya hivi kama sehemu ya kujali na kuchangia maendeleo ya jamii,” aliongeza Meneja huyo.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igawilo, Donald Mwashtete, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo pamoja na Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, aliishukuru Shirika la Posta kwa kitendo hicho cha kuikumbuka hospitali yao.
“Tunawashukuru sana wenzetu wa Shirika la Posta kwa kutukumbuka na kufanya jambo hili jema. Ni ishara ya upendo na ushirikiano mzuri kati ya taasisi za umma. Kwa niaba ya wagonjwa na wateja wetu, tunasema asanteni sana kwa zawadi hizi ambazo zitawasaidia walengwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Mwashtete.
Ameongeza kuwa msaada huo umewatia moyo watumishi wa afya na kuonyesha namna taasisi za umma zinavyoweza kushirikiana kwa manufaa ya wananchi.
“Tunathamini sana mchango huu, kwani unaonyesha dhamira njema ya Serikali kupitia Shirika la Posta katika kusaidia jamii na kuboresha huduma za afya,” alimalizia.