Rungwe, Tanzania – Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe imekamilisha hatua ya awali ya mradi mkubwa wa Soko la Kisasa la Ndizi lenye thamani ya Shilingi bilioni 2.8, hatua inayofungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa wakulima na wafanyabiashara wa eneo hilo na mikoa ya jirani.
Akizungumza wakati wa hafla ya leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Bwana Renatus Mchau, amesema hatua hii ni kumkabidhi mkandarasi site pamoja na kuhakikisha taratibu zote za kimkataba zimekamilika.
“Leo hii tumekamilisha taratibu zote za kimkataba. Zoezi la leo ni kumkabidhi mkandarasi site, kuhakikisha kila kitu kipo sawa kabla ya kuanza ujenzi rasmi,” alisema Mchau.
Mkurugenzi Mtendaji aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wizara ya Tamisemi, Wizara ya Fedha, na Wizara ya Kilimo kwa mchango wao wa kitaalam katika hatua zote za maandalizi ya mradi. Alihakikisha kuwa wananchi, wafanyabiashara na wakulima ambao kwa muda mrefu wamepitia changamoto mbalimbali katika eneo hilo, wanapaswa kuwa wanufaika wakubwa wa mradi huu. 
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Kagwa General Supplies Limited, Bwana Emmanuel Madaffa, amesema serikali imeonyesha imani kubwa kwa kutoa fursa kwa wazawa kutekeleza mradi huo badala ya wageni.
“Naiishukuru sana Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini sisi wazawa. Tunawaahidi kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunatimiza lengo la Serikali na kuondoa changamoto za muda mrefu kwa wananchi,” alisema Madaffa.
Amesema mradi huo utakuwa kichocheo muhimu cha maendeleo na utawanufaisha si tu wakulima wa Rungwe na Kyela, bali pia mikoa ya jirani. Kampuni tayari imekabidhiwa cheti cha kuanza kazi, hivyo shughuli zinaanza mara moja. Aidha, amewaasa wakandarasi kushirikiana na wahandisi na taasisi za kitaalamu, kuepuka ubadhirifu, na kutoa nafasi kwa vijana wa Rungwe kushiriki katika kazi ndogo zisizohitaji ujuzi.
Mbunge wa Jimbo la Rungwe, Mh. Mantona, amesema soko hilo ni mojawapo ya miradi mikubwa inayolenga kuboresha uchumi wa wakulima na wafanyabiashara wa eneo hilo, akibainisha kuwa litafungua fursa nyingi za kipato na kuongeza thamani ya mazao.
“Huu ni mradi mkubwa sana kwa watu wa Rungwe. Tukiuendeleza vizuri, manufaa yake yataonekana kwa wote—wakulima, wafanyabiashara, na jamii kwa ujumla,” alisema Mbunge Mantona.
Soko hili la kisasa linatarajiwa kuwa suluhu ya kudumu kwa changamoto ya masoko kwa wakulima wa ndizi, litakaloongeza thamani ya zao hilo, na kuvutia wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Mwisho, Afisa Tawala Amimu Mwandelile, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya Rungwe, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwazi na kufuata taratibu zote za kiserikali katika utekelezaji wa mradi.
“Njia bora ya kutatua changamoto ni kupitia vikao na majadiliano ya pamoja. Viongozi, wafanyabiashara na wahandisi wanapaswa kushirikiana ili mradi uendelee bila matatizo,” alisema Mwandelile.
Amewaasa wakandarasi kushirikiana na taasisi za kitaalamu, kuzingatia mkataba, na kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa viwango vinavyotarajiwa. Pia alisisitiza kuepuka haraka isiyo na mpangilio, ubadhirifu au ubinafsi, akibainisha kuwa kila hatua inapaswa kufuata mpangilio thabiti ili kufanikisha mradi.
“Tukiongoza mradi huu vizuri na kushirikiana kwa uwazi, tutapata matokeo bora. Mradi ni mali ya wananchi na kila mmoja ana wajibu wa kulinda ubora wake,” aliongeza.





