Wakazi wa Mkoa wa Mwanza wakiwa katika vituo vya Kuboreshea Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakijiandisha na kuboresha taariza zao leo ambapo uboreshaji huo umeanza kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Mikoa hiyo itafanya zoezi hilo kwa siku saba kuanzia leo Agosti 21 hadi 27, 2024.
Wakazi wa Mkoa wa Mwanza wakiwa katika vituo vya Kuboreshea Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakijiandisha na kuboresha taariza zao leo ambapo uboreshaji huo umeanza kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Mikoa hiyo itafanya zoezi hilo kwa siku saba kuanzia leo Agosti 21 hadi 27, 2024.
Vijana ni kundi kubwa la Wananchi ambao wameanza kujitokeza kwa wingi vituoni kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari (wapili kulia) akikagua zoezi la uboreshaji lililoanza leo Mkoani Mwanza ambapo alitembelea vituo mbalimbali katika majimbo ya Magu, Ilemela na Nyamagana mkoani humo.Kulia ni Afisa Mwandikishaji Msaidizi ngazi ya Kata kutoka Kata ya Buswelu Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Godson Egubo wakiwa katika kituo cha Shule ya Msingi Eden Valley.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari akikagua zoezi la uboreshaji lililoanza leo Mkoani Mwanza ambapo alitembelea vituo mbalimbali katika majimbo ya Magu, Ilemela na Nyamagana mkoani humo.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari akikagua zoezi la uboreshaji lililoanza leo Mkoani Mwanza ambapo alitembelea vituo mbalimbali katika majimbo ya Magu, Ilemela na Nyamagana mkoani humo.
Afisa Mwandikishaji Msaidizi ngazi ya Kata ya Buswelu Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Godson Egubo (kushoto) akikagua mwenendo wa zoezi la Uboreshaji katika Kituo cha Shule ya Msingi Eden Valley kilichopo katika Kata yake.
Na Mwandishi wetu, Mwanza
Wakazi wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga wamejitokeza kwa wingi katika siku ya kwanza ya zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanza leo Agosti 21 na litaendelea hadi Agosti 27,2024.
Mwandishi wa habari hii, ameshuhudia uwepo wa wananchi wengi vituoni haswa vijana na wanawake waliojitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa tathmini ya mwenendo wa zoezi hilo kwa siku ya kwanza Mkoa wa Mwanza, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari amesema zoezi limeanza viziri na mwitikio wa wananchi ni mkubwa.
“Leo siku ya kwanza zoezi limeanza vizuri ambapo wananchi wamejitokeza, mawakala wapo vituoni na nimebahatika kuzungumza na mawakala, watendaji vituoni na wananchi. Kwa ujumla zoezi linakwenda vizuri,”amesema Jaji Asina.
Aidha, Jaji Asina amesema changamoto zilizojitokeza ni za kawaida na zinatatulika lakini changamoto kubwa ni wananchi wanaofika kuboresha taarifa zao kusahau majina waliyoyatumia awali kujiandikishia namna yanavyoandikwa kwa usahihi, hivyo inapelekea uchelewaji vituoni.
Amesema makundi mbalimbali ya wanawake wajawazito, wanaonyonyesha na kufika na watoto wao vituoni, Wazee, Wagonjwa na wenye ulemavu wameendelea kupewa kipaumbele kama Tume ilivyoelekeza.
Jaji Asina ambaye alifanikiwa kutembelea baadhi ya vituo katika Majimbo ya Magu, Nyamagana na Ilemela amewaasa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa siku sita zilizobaki na wasisubiri siku ya mwisho.
“Niwasihi wananchi wajitokeze katika vituo ili waweze kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ambapo katika vituo tumeona vijana wengi, hivyo watumie siku hizi zilizobaki kuboresha taarifa zao na kuajindikisha,amesema Jaji Asina.
Mjumbe wa Tume, Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri ambaye yupo Mkoani Shinyanga amesema mkoani humo zoezi hilo limeanza vizuri na wananchi wengi wamejitokeza kujiandikisha kwa wingi.
Mawakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Paul Msafiri na Wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Lydya Martin waliopo kituo cha Bulola Mlimani kilichopo eneo la Zahanati ya Nyerere katika Halmashauri ya Ilemela wamesema zoezi hilo linakwenda vizuri na hakuna changamoto iliyojitokeza.
Aidha, wakala Fatuma Athumani wa Chadema aliyopo kituo cha Miembeni A kilichopo eneo la wazi Nyakabungo A katika Halmashauri ya Jijini la Mwanza amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata haki yao ya kuwa na kadi ya Mpiga Kura.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga limeanza leo Agosti 21 hadi Agosti 27,2024 ambapo Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 400,082 kwenye mikoa hiyo.
Mkoani Mwanza wapiga kura wapya 190,131 wataandikishwa huku Shinyanga wapiga kura wapya wanaotarajiwa kuandikishwa ni 209,951.