Afisa anayeshughulikia malamiko Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za nishati na maji(EWURA)Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Francis Mhina amesema taasisi yake imerahisisha upatikanaji vibali vya ujenzi wa vituo vya mafuta maeneo ya mijini na vijijini.
Ameyasema hayo katika maonesho ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu yanayofanyika katika Uwanja wa John Mwakangale Jijini Mbeya.
Katika hatua nyingine Mhina amesema mwananchi mwenye malalamiko juu ya utendaji usioridhisha kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira,Shirika la Umeme na Vituo vya mafuta ofisi yake ipo wazi kupokea changamoto hizo.
Ofisi ya EWURA imeyatumia maonesho ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za juu ili wananchi kutoka Mikoa mingine waweze kujionea na kujifunza shughuli zinazotekelezwa na Taasisi hiyo ya umma.
Tobieta Makafu Afisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za nishati na maji(EWURA)Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inahudumia Mikoa ya Mbeya,Njombe,Songwe na Rukwa amesema endapo mwananchi atauziwa mafuta kinyume na bei elekezi asisite kutoa taarifa EWURA.
Amesema kila jumatano ya kila mwezi EWURA hutoa bei elekezi kupitia vyombo vya Habari na simu za mkononi.
Bado jamii haijapata elimu ya kutosha juu ya uwasilishaji wa malalamiko pindi wanapokutana na changamoto.