Kambi ya wiki moja ya uchunguzi na upasuaji mtoto wa jicho iliyoanza juni 18,2024 hadi juni 24,20224 katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya kwa ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la Helen Keller International na Wizara ya Afya imepata mafanikio makubwa baada kufurika wagonjwa wengi kuhitaji huduma hiyo kinyume na matarajio yao lengo ilikuwa ni kuwafikia wagonjwa mia nne hamsini baada ya kufanyiwa uchunguzi katika Kata kumi na saba kati ya Kata ishirini za Wilaya ya Chunya.
Akitoa taarifa baaada ya kutamatika kambi hiyo iliyojumuisha Madaktari wa macho kutoka Hospitali mbaalimbali nchini chini ya Daktari Bingwa wa macho Hospitali ya Ruufaa Kanda ya Mbeya Dkt Barnabas Mshangila,Athuman Tawakal Meneja wa Maradi kutoka Shirika la Helen Keller International amesema wagonjwa waliofanyiwa uchunguzi wa awali ni wagonjwa mia tano thelathini na tatu (533) na lengo la upasuaji likiwa ni wagonjwa mia nne hamsini(450) ambapo mwisho ya kambi hiyo wamefanya upasuaji wa macho mia nne hamsini na tisa (459) ikiwa nii rekodi ya kwanza tangu kuanza kambi za macho katika mikoa ya Mbeya,Songwe na Njombe.
“Katika kambi hii rekodi tuliyoiweka wenyewe tumeivunja wenyewe hii ni kutokana na kuendelea kuimarika ujuzi kwa madaktari na wauguzi hasa baada ya kujengewa uwezo na matumizi ya vifaa vya kisasa vilivyofungwa katika hospitali mpya za Wilaya zilizojengwa na serikali nchini hali inayowapa urahisi madaktari kutekeleza majukumu yao”alisema Tawakal.
Hata hiivyo Tawakal amewaomba wadau wengine kuungana na Hellen Kelller ili waweze kuwafikia watu wengi zaidi kwani peke yao hawawezi kuwafikia wagonjwa wote kutokana na uhaba wa raslimali fedha.
Dkt Greter Mande kutoka Mpango wa Huduma za Macho Wizara ya Afya ameomba wananchi kuitumia fursa hiyo ya matibabu ya bure huku akilipongeza Shirika la Helen Keller International kwa kugharamia matibabu bure kwani wananchi wengi wasingeweza kugharamia usafiri na matibabu kutokana na changamoto za uchumi pia mila potofu baadhi wakidai ugonjwa huo unatokana na kulogwa.
Kambi hiyo ilitembelewa pia na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt Elizabeth Nyema mbali ya kulishukuru Shirika la Helen Keller International kwa kufadhili matibabu ameipongeza Wizara ya Afya na Madaktari kusimamia zoezi la matibabu amballo limefanyika kwa ufanisi mkubwa likiongozwa na madaktari wazalendo.
Amelitaka Shirika la Helen Keller International kuendelea kuwasaidia wananchi hasa walioko pembezoni ambao hawawezi kugharamia usafiri,uchunguzi na matibabu ya mtoto wa jicho.
Naye Mganga MKuu wa Wilaya ya Chunya Dkt Darison Andrew amesema huduma hiyo imewapunguzia gharama wagonjwa wa mtoto wa jicho ambapo wagonjwa walilazimika kuifuata Hospitali ya Mkoa wa Mbeya au Hospitalli ya Rufaa Kanda ya Mbeya na wengi wao walishindwa gharama za usafiri huku wakiamini hayo ndiyo maisha waliyouumbiwa.
Amesema haya ni mafanikio makubwa katika Wilaya yake mbali ya wagonjwa kunufaika na matibabu watumishi wa kitengo cha macho wamepatiwa ujuzi watakaoutumia hata baada ya kutamatika kambi hiyo.
Aidha Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya Dkt John Gungumka amesema matibabu ya mtoto wa jicho gharama yake ni kubwa hivyo ameomba huduma hiyo iwe endelevu na imewajengea uwezo watumishi wa hospitali hiyo.
Akitamatisha kambi hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Tamim Kambona mbali ya kupongeza ufanisi mkubwa wa huduma ya Madaktari na Wataalam wazalendo ameliomba Shirika la Helen Keller International kuendelea kuisaidia Wiilaya ya Chunya kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma ya matibabu ya mtoto wa jicho na Kata tatu bado hazijafikiwa na huduma hiyo.
“Huu usiwe mwisho wwa kufika Wilaya ya Chunya kwani mazingirra ya kazi ni rafiki kutokana na serikali kuendelea kuboresha majengo na ununuzi wa vifaa tiba ili kuwapatia wananchi huduma bora za matibabu”alisema Kambona.
John Mpozayo (73), mkazi wa Saza Wilaya ya Songwe, ni miongonimwa waliokuwa wakisumbuliwa na mtoto wa jicho kwa miaka mitano. Ameeleza changamoto za kutoona zilivyomzuia kuhudhuria kanisani na kufanya shughuli nyingine, na jinsi alivyokuwa akimtegemea mkewe kwa msaada wa kumwongoza.
Mzee Mpozayo alieleza kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Chunya,ameonekana mwenye furaha na ametoa shukrani zake kwa serikali na Shirika la Helen Keller International.
Wilton Mkongoma, mwenye umri wa miaka 80 na mkazi wa Rungwa, amepata matibabu ya mtoto wa jicho katika kambi maalumu ya macho iliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kutoka Juni 19 hadi Juni 24, 2024. Mkongoma, aliyekuwa haoni kwa zaidi ya miaka miwili, alipata taarifa za kambi hiyo kupitia watu waliotibiwa macho Makongolosi. Baada ya kupokelewa na kupimwa, ilithibitishwa kuwa ana tatizo la mtoto wa jicho na alifanyiwa matibabu ambayo yalimwezesha kuona tena.
“Nimezaliwa upya sasa naona,” alisema Mkongoma kwa furaha. Mkongoma amesema hajawaona ndugu zake kwa miaka miwili na nusu na sasa amefurahi kuwaona tena pamoja na mifugo yao.
Mwajuma Bahati (20)mkazi wa Kijiji cha Mamba E Kata ya Mamba Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya alianza kusumbuliwa na mtoto wa jicho akiwa darasa la sita.Analishukuru Shirika la Helen Keller kwa kumpatia matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
Meshack Cheyo (16) mkazi wa Sagambi Chunya ambaye alipata jeraha la jicho baada ya kuumia akicheza na wenzake ni miongoni mwa watu waliopatiwa matibabu kwenye kambi ya matibabu iliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
Israel Victor Haule(58)mwalimu mstaafu mkazi wa Ujenzi Kata ya Itewe Wilaya ya Chunya amelishukuru Shirika la Helen Keller International kwa kumsaidia matibabu bure.”Nilikuwa siwezi hata kurudisha chenji dukani kutokana na kusumbuliwa na macho ambapo nilipoteza uwezo wa kuona kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa”alisema mwalimu Haule huku akitabasamu.
Epyphania Nicholaus (40 )mkazi wa Mamba Wilaya ya Chunya alianza kusumbuliwa na macho akiwa darasa la sita na alipomaliza darasa la saba hali ilikuwa mbaya zaidi na sasa amepatiwa matibabu ambapo amelishukuru Shirika la Hellen Keller kufanikisha matibabu.Masanja Magulu mkazi wa Matondo Itumbi Kata ya Matundasi alipata jeraha la jicho baada ya kuchomwa na mwiba akiwa katika machungo ya ng’ombe amelishukuru Shirika la Hellen Keller na madaktari kwa kumpatia matibabu ya mtoto wa jicho kambi iliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wamewapongeza wafaddhilii wa Shirika la Helen Keller kwani wengi wao walikata tamaa ya maisha kutokana na utegemezi kwenye familia zao kwani baadhi umri wao ni mdogo hivyo kitendo cha kukumbwa na maradhi kulisababisha mdororo wa kiuchumi.
Shirika pia kwa kuona umuhimu limekuwa likigharamia matibabu kwa watoto baadhi yao walikatiza masomo lakini baaada ya kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho wamerejea shule hivyo kufufua ndoto zao za kimaisha.
Shirika la Helen Keller limeanza kutoa huduma Kanda ya Nyanda za Juu katika Mikoa ya Mbeya, Njombe na Songwe likijikita zaidi kwa wagonjwa wa vikope na mtoto wa jicho ambapo baadhi ya wagonjwa walipoteza uoni na kuwa vipofu.