Na Mwandishi `Maalumu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa maono yake ya mbali na uamuzi wa busara wa kumpendekeza Profesa Mohamed Yakub Janabi kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Wananchi mbalimbali waliohojiwa wametaja hatua hiyo ya Rais Samia kama ishara ya kujiamini kama taifa, na uthibitisho kuwa Watanzania wanao uwezo wa kushika nafasi nyeti katika taasisi kubwa za kimataifa, wakielezea faraja yao kwa jinsi Tanzania inavyozidi kung’ara kwenye majukwaa ya kidiplomasia duniani.
Aidha, Rais Samia amesifiwa kwa kuunda kikosi kazi maalum kilichoongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa ajili ya kuratibu na kusimamia kampeni ya kidiplomasia ya Profesa Janabi.
Ushirikiano huo umeibuka na matokeo chanya, ambapo Profesa Janabi ameibuka mshindi kwa kishindo kupitia mchakato wa uchaguzi uliopigiwa kura na nchi wanachama wa WHO Kanda ya Afrika.
Dkt. Kikwete, ambaye ana uzoefu mkubwa katika medani za kimataifa, amepongezwa kwa kutumia umahiri na uhusiano wake wa kidiplomasia kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa. Mchango wake umetajwa kama kichocheo muhimu kilichowezesha Tanzania kupata ushindi dhidi ya wagombea kutoka Côte d’Ivoire, Guinea na Togo.
Katika picha iliyopigwa wakati wa harakati za kampeni hiyo, Dkt. Kikwete anaonekana akiongoza moja ya vikao vya kikosi kazi hicho, ambacho hatimaye kilitimiza azma yake mnamo Jumapili, Mei 18, 2025, kwa ushindi mkubwa wa Profesa Janabi.
Mgombea huyo wa Tanzania alipata kura 32 kati ya 47 zilizopigwa kwa siri na wajumbe wa nchi wanachama wa WHO Afrika, kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa WHO.
Uchaguzi huo umefanyika kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule, Dkt. Faustine Ndugulile, mnamo Novemba 2024. Nafasi hiyo ilivuta wagombea mahiri kutoka mataifa kadhaa, lakini Profesa Janabi alifanikiwa kuungwa mkono kwa wingi, akionesha kuwa jina la Tanzania bado lina nguvu katika diplomasia ya afya barani Afrika.
Kwa mujibu wa taratibu za Shirika la Afya Duniani, jina la Profesa Janabi sasa litawasilishwa kwa ajili ya kuthibitishwa rasmi na Bodi ya Utendaji ya WHO katika kikao chake cha 157 kitakachofanyika Mei 28–29, 2025, mjini Geneva, Uswisi.
Iwapo atathibitishwa, Profesa Janabi ataapishwa na kuanza kutekeleza rasmi majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitano, huku akiwa na fursa ya kuongezewa muhula mmoja zaidi kulingana na kanuni za taasisi hiyo.