Stephen Samuel Langeni, Mkurugenzi wa Maranatha Pharmacy na Maranatha Hospitali, ambaye pia ni Mwakilishi wa Wafanyabiashara Mkoa wa Mbeya, ametoa rai kwa viongozi na wananchi wa mkoa huo kushirikiana kulinda na kutunza rasilimali za kijani ambazo ndiyo fahari ya Mbeya.
Akizungumza katika kikao maalum, Langeni alisema jina la Mbeya limekuwa likihusishwa moja kwa moja na mandhari ya kijani, lakini hali hiyo ipo hatarini kupotea kutokana na changamoto za ukataji miti holela pamoja na mwamko mdogo wa upandaji miti.
“Mbeya imekuwa ikitambulika kama fahari ya kijani, lakini sasa sifa hii inaondoka kwa kasi kubwa. Kila siku miti mingi inakatwa, na hatua za upandaji hazilingani na kiwango cha ukataji,” alisema Langeni.
Aidha, alieleza kuwa wananchi wengi husikitishwa wanaposhuhudia miti ya zamani inayopendezesha barabara na mandhari ya mji ikikatwa bila taarifa rasmi.
“Miti ambayo imekuwa sehemu ya fahari ya wananchi inapoondolewa, wananchi hawapati taarifa yoyote. Tunashauri kuwe na utaratibu wa kisheria na matangazo ya wazi kabla ya mti wowote kukatwa, ili wananchi wajue sababu na pia wajadili kama kuna njia mbadala,” aliongeza.
Langeni alisisitiza kuwa mbali na kampeni za upandaji miti, ni muhimu zaidi kujenga utamaduni wa kutunza na kulinda miti iliyopo. Aliahidi kuwa Jumuiya ya Wafanyabiashara iko tayari kushirikiana na Serikali kufanikisha kampeni hizo kwa kugharamia miche, kugawa miti, na kusimamia zoezi hilo nyumba kwa nyumba.
Mbali na suala la miti, Langeni pia aligusia changamoto za taa za barabarani, akisema baadhi zimeharibika huku zingine zikihitaji huduma ndogo tu za matengenezo.
“Ni vyema tukatambua ni taa zipi zimeharibika kabisa na zipi hazijafanyiwa huduma. Zikifanyiwa matengenezo, tutaurejesha mji wetu katika mwanga, na mwanga huo utaendana na mandhari yetu ya kijani,” alisema.
Langeni alimalizia kwa kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa hatua alizochukua, huku akisisitiza umuhimu wa kufuatilia utekelezaji wa kampeni za upandaji na utunzaji miti hadi ngazi za mitaa na kaya.