Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Benno Malisa amewaalika wawekezaji kuwekeza katika mkoa wa Mbeya kwenye fursa za Biashara, Usafirishaji, Viwanda, Ufugaji, Utalii na uwekezaji kwenye mifumo ya Kidijitali.
RC Malisa ameyasema hayo kwenye mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu TIA Kampasi ya Mbeya kwenye kilele cha mahafali ya Taasisi hiyo.
Jumla ya wahitimu 1480 wa ngazi mbalimbali ya vyeti, Astashahada na Shahada wamehitimu katika Taasisi hiyo.
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza mkoani kwetu kwenye miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea, imeongeza mvuto wa uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi” Amesema RC Malisa.
Aidha RC Malisa amesema mkoa wa Mbeya ni kati ya mikoa yenye fursa kwenye ubunifu na ukuaji wa kibiashara hivyo wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa nia ya kuanzisha safari yao ya ubunifu na ujasiriamali.
Amewataka wahitimu wa Taasisi hiyo kuwa wabunifu kwa kutengeneza mawazo na suluhisho wenye ubunifu ili kuibua changamoto zilizopo katika jamii.
Pia RC Malisa amewataka wahitimu kutumia teknolojia kwa tija ili teknlolojia ibebe biashara, mawazo na huduma wanazozitoa na kutakiwa kuitumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujipatia kipato.
Awali akizungumza wakati akimlaribisha mgeni rasmi, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania TIA Prof William Pallangyo Taasisi ya Uhasibu Tanzania imeanzisha kozi mpya tatu za masomo ya juu (Post Graduate),Ngazi za Shahada(Bachelor degree)ili kuendana na soko la ajira lililopo kwa sasa nchini.
Amesema mkoani Mbeya Taasisi ya Uhasibu Tanzania imeanzisha Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uhasibu wa Fedha, Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Ununuzi na Ugavi, Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara katika Usimamizi wa miradi, Shahada ya Uongozi wa Rasilimali watu na Shahada ya Biashara.
Prof Pallangyo amesema Kozi zilizozinduliwa na RC Malisa katika mahafali ha hayo ni fursa kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya, mikoa ya jirani na nchi jirani za Malawi na Zambia.
Aidha Prof Pallangyo amesema kubwa katika kuwa kuwaendeleza wanachuo kupitia kitengo cha Uendelezaji wanachuo kitaalamu na kitaaluma wameandaa shindano la Ubunifu, mshindi wa kwanza kutoka kila Kampasi kwa mwaka 2025-26 atapata fursa kutembelea Chuo kikuu cha Pretoria Nchini Afrika Kusini kwa ajili ya ziara ya kimafunzo na kujipatia uzoefu.


