Madaktari Bingwa wa Mifupa na Magonjwa yanayohusiana na Ajali kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo wameanza kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa mkoani Manyara katika kambi maalumu ya Madaktari Bingwa ya Mifupa, Macho, pua, koo na masikio iliyoandaliwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, inayolenga kusogeza na kuboresha huduma kibingwa za afya kwa wananchi wa mkoa wa huo.
Kwa upande wake, Dkt Baraka Mponda, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa kutoka Rufaa ya Kanda Mbeya, amesema kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali na Wadau wa afya wa kuhakikisha huduma za matibabu zinawafikia wananchi popote walipo.
“Tunataka kuhakikisha kuwa wagonjwa wanapata huduma bora za kibingwa bila usumbufu, kubadilishana na kujengeana uwezo kwa watoa huduma za afya na pia hii ni sehemu ya juhudi zinazozingatia ushirikiano kati ya hospitali za Mikoa na zile za Kanda, ili kuhakikisha huduma za kibingwa zinapatikana kwa urahisi zaidi kwa wananchi wa Manyara na maeneo jirani,” alisema Dkt. Mponda
Kambi hii maalum inayofanywa kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya itadumu kwa siku tano kuanzia Januari 26 hadi 30, 2026, ambapo madaktari bingwa hao watafanya kliniki za matibabu, upasuaji, na ushauri wa kitaalamu kwa wagonjwa wenye matatizo ya mifupa na ajali.

