Author: Mbeya Yetu

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile, kimeacha simanzi kubwa kwa Bunge na Watanzania kwa ujumla kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mtaa wa Uzunguni A, Jijini Mbeya leo tarehe 27 Novemba, 2024, Dkt. Tulia amesema kuwa nyota ya Dkt. Ndugulile imezimika wakati akiwa ameanza kung’ara katika anga za kimataifa. Alikuwa aanze rasmi majukumu yake mapya ya kimataifa mwezi Machi mwaka 2025.

Dkt. Tulia amesema kuwa Bunge limepoteza Mbunge mahiri ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI. Mchango wake uliwezesha kufanikisha mabadiliko makubwa ya sheria na sera katika sekta za afya na mapambano dhidi ya UKIMWI.

Aidha, amewataka Wananchi wa Kigamboni kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho wamempoteza Mbunge wao na kumuombea apumzike kwa amani.

Dkt. Ndugulile amefarikidunia usiku wa kuamkia leo nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Read More

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Ramadhan Tembo Mwakilasa [28] na Mariamu Charles Mwashambwa [28] wote wakazi wa TEKU viwandani Jijini Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Chloy Ramadhan [04] kwa kumpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili.

Ni kwamba Novemba 25, 2024 saa 2:00 usiku huko Mtaa wa TEKU viwandani Jijini Mbeya, mtoto Chloy Ramadhan [04] alifariki dunia baada ya kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi aitwaye Ramadhan Tembo Mwakilasa [28] akishirikiana na mama yake wa kambo aitwaye Mariamu Charles Mwashambwa [28] wote wakazi wa TEKU viwandani.

Uchunguzi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ukatili na unyanyasaji kwa kumuadhibu mtoto baada ya kujisaidia kwenye nguo alizokuwa amezivaa.

Jeshi la Polisi linawataka wazazi/walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watoto pindi wanapokosea na badala yake watumie njia sahihi na salama kuwafundisha au kuwaelekeza bila kusababisha madhara.

Read More