REGROW ni Mradi wa Serikali unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa Lengo la kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na hifadhi ya Mikumi, Udzungwa na Nyerere wanatekeleza mradi huu. Kutokana na utekelezaji wa mradi wa REGROW au shughuli za Hifadhi ya Taifa Ruaha, unaweza kuwa na maoni au malalamiko yanayotokana na shughuli hizo.
Kila mtu ana nafasi ya kutoa malalamiko yake kuhusu changamoto zinazotokana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na shughuli za Mradi wa REGROW. Iwe malalamiko ya athari zinazotokana na usimamizi wa hifadhi, kero za ardhi, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia au kuhusu migogoro ya wanyamapori wakali na waharibifu, na kadhalika.
Je una lalamiko lolote kuhusu mradi wa REGROW? Na je, unafahamu unafikishaje malalamiko yako?
Kuna njia tatu rahisi za kufikisha malalamiko yako:
Kwanza unaweza kutembelea ofisi za kijiji chako na kuwasilisha malalamiko yako hapo. Yatapokelewa na kushughulikiwa kupitia Mfumo wa Kushughulikia Malalamiko.
Njia ya pili, unaweza kupiga simu bure kwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kupitia namba 0 800 110 801 au katika Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia 0 800 110 804.
Lakini pia unaweza kutuma malalamiko yako kupitia mfumo wa Serikali wa e- Mrejesho mtandaoni kwa kutembelea www.emrejesho.gov.go.tz, au piga *152*00# kisha chagua 9, alafu chagua 2 ili kuufikia mfumo wa e-Mrejesho. Hapo utaweza kutoa malalamiko yako.
Kumbuka, malalamiko yako yatapokelewa kwa usiri ili kukulinda kama mlalamikaji. Na yeyote atakayemdhuru mlalamikaji kwa namna yeyote atachukuliwa hatua za kisheria. Malalamiko yatasikilizwa kwa umakini, na utapata mrejesho mara moja. Hifadhi ya Taifa Ruaha na Mradi wa REGROW wanahakikisha usalama na ustawi wa jamii yako.