Kazi ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wanaotembelea banda la Mama Samia Legal Aid Campaign, ikiendelea kwenye maonesho ya nanenane jijini Dodoma
Na Mwandishi Wetu
BAADA ya kusaidia maelefu ya Watanzania kupitia maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia au maarufu kama Mama Samia Legal Aid Campaign, sasa iko katika maonesho ya nanenane jijini Dodoma.
Kampeni hiyo ambayo tangu kuzinduliwa kwake mwaka jana, imekuwa ikitumia wabobezi katika tasnia hiyo ya sheria kutatua migogoro mbalimbali inayotokea kwenye jamii katika mikoa mbalimbali wanakopita iko katika maonesho hayo kutoa msaada huo wa kisheria kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo ya nanenane.
Mbali na kurejesha tabasamu kwa wananchi wenye migogoro mbalimbali, pia kampeni hiyo imefanyika kama darasa la kutoa elimu kuhusu masuala ya sheria na namna haki inavyoweza kupatikana kwa kutumia sheria hizo.
Kampeni hiyo ya Mama Samia Legal Aid Campaign katika maonesho hayo, pia inalenga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za ushauri na ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya kisheria wanayokumbana nayo katima maisha yao ya kila siku.
Kampeni hiyo inatoa fursa kwa wananchi kukutana na wataalamu wa sheria ambao wanaweza kuwasaidia kuelewa na kutatua matatizo yao na wanapata nafasi ya kushauriana na wanasheria bila gharama yoyote.
Miongoni mwa maeneo wanayoweza kupatiwa msaada wa kisheria ni pamoja na yale ya kifamilia, mirathi na mengineyo.
Kampeni hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika kwa miaka mitatu mpaka mwaka 2026 Februari katika pande zote mbili za Muungano, tayari imewafikia wananchi zaidi ya 500,000 katika mikoa saba ya Dodoma,Singida, Shinyanga, Simiyu, Manyara, Njombe na Ruvuma ambako tayari jopo la wasaidizi wa kisheria kutoka katika kampeni hiyo limepita.