Wakazi wa mtaa wa Gombe kusini kata ya Itezi Uyole jijini Mbeya, wanakabiliwa na ukosefu wa huduma ya maji kwa zaidi ya miaka minne sasa hivyo kuitaka Serikali kutupia jicho kadhia hiyo.
Wananchi wa mtaa huo wamesema hayo kwenye ziara ya wataalam wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Mbeya ambao wamelazimika kutoka ofisini kwenda mtaani kujionea hali halisi ya upatikanaji huduma ya maji na hatua zinazochukuliwa.
Wakizungumza mbele ya wataalam hao kwa nyakati tofauti, wananchi hao akiwemo Tuswege Ngondo na Elly Mwampamba, wanasema huduma ya maji wameikosa kwa muda mrefu wengine kwa mwaka mmoja lakini wengine ni zaidi ya miaka minne.
Bi. Tuswege Ngondo mkazi wa mtaa huo, anasema “Nashukuru kwasababu mmekuja lakini maji ni changamoto kubwa hata mwenyekiti wangu wa mtaa hana maji kwake sasa mtwambie sisi ni wa Ethiopia halafu wenzetu wa mitaa mingine ndio wa-Tanzania kwasababu hatuelewi”.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Gombe kusini Obedy Mandalasi, anasema maji limekuwa tatizo sugu mtaani kwake hatua inayowalazimu wananchi wake kununua.
“Unakuta mtu ananunua maji mfano mimi kwa siku lazima ninunue maji ya elfu mbili au elfu tatu kila siku unakuta pipa moja unatumia kwa siku limeisha kwahiyo ujio wenu kwetu tunaamini ni neema”, ameeleza mwenyekiti wa mtaa.
Akijibia kero hiyo kuu ya wakazi wa Gombe kusini, kaimu mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya Mhandisi Barnabas Konga, amesema mamlaka imeamua kutoka ofisini ili kuwafikia wateja wake na kuwaeleza mipango iliyopo ili kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa tatizo la maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mbeya ikiwemo Gombe kusini na Ituha.
Amesema Serikali kupitia mamlaka ya maji, imeanza utekelezaji wa mradi wa Halinji Nsalaga mradi ambao utanufaisha wananchi hadi mtaa wa Gombe kusini ambapo pia kwa hatua za awali na za muda mfupi tayari kisima kilishachimbwa katika eneo la shule ya msingi Gombe ili kusaidia kupunguza kadhia ya maji kwa wananchi hao.
Mhandisi Konga amewatoa hofu wananchi wa Gombe kusini kuwa mamlaka kupitia mapato yake ya ndani pamoja na fedha kutoka Taifa watahakikisha kilio cha maji kinakuwa historia hivi karibuni kutokana na ukweli kwamba Halmashauri ya jiji la Mbeya imekuwa na ongezeko la watu kila uchao.