CPA. Gilbert Kayange, Mkurugenzi Mtendaji wa MBEYA-UWSA, amefanya ziara ya mtaa kwa mtaa katika Jiji la Mbeya kukagua miundombinu ya maji, kusikiliza kero na kutatua changamoto mbalimbali za kihuduma kwa wateja.
Katika zoezi hilo, CPA. Kayange amepokea changamoto mbalimbali zikiweko uwepo wa wizi wa mita za maji kwa baadhi ya wateja, na baadhi ya Wananchi wasio waaminifu kuingilia miundombinu ya maji kwa makusudi ili kujipatia huduma ya maji kinyume cha Sheria.
Akijibu changamoto hizo, CPA. Kayange ameeleza kwamba, Mbeya-UWSA inatambua uwepo wa changamoto hizo na kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama tayari baadhi ya watuhukiwa wa vitendo hivyo wamefikishwa Mahakamani kwa kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Aidha, CPA. Kayange ametoa wito kwa Wananchi kushirikiana na Mbeya-UWSA kwa kutoa taarifa ya wizi wa maji na wizi wa mita na kwamba atakayembaini mhalifu atapewa donge nono la Shilingi za Kitanzania Milioni Moja (1,000,000/=).
Uharibifu wa miundombinu ya maji huleta hasara kwa Serikali kwani vitendo hivyo husababisha upotevu wa maji, upotevu wa mapato , huongeza gharama za uendeshaji na kuathiri upatikanaji wa huduma bora na endelevu kwa Wananchi.