Na Mwandishi wetu Dar.
Mwenyekiti Mstaafu wa Serikali ya Mtaa wa Sangara Kata ya Msongola wilaya ya Ilala jijini Dar esSalaam Pili Charles Ndimaye amejiunga na Chama Cha ACT Wazalendo baada ya kumaliza muda wake wa uongozi Oktoba 19 Mwaka huu.
Taarifa ya viongozi wa ACT Wazalendo Jimbo la Ukonga iliyotolewa leo (Oktoba 22, 2024), imeeleza kuwa Ndimaye amejiunga na Chama hicho Oktoba 19, 2024 ikiwa ni muda mchache baada ya kumaliza taratibu za kukabidhi Ofisi ya Mtaa kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Tamisemi Mohamed Mchengerwa.
Akizungumza Kwa njia ya simu na Mwandishi wa Habari hizi, Mwenyekiti wa ngome ya wazee Jimbo la Ukonga Bakari Shingwe, amesema Ndimaye amesajiliwa na Chama hicho akiwa ni kiungo muhimu kuhakikisha ACT inashinda katika Kata ya Sangara na Jimbo la Ukonga Kwa Ujumla.
“Hivi karibuni viongozi wetu wa kitaifa walikuwa na ziara mikoani kwa ajili ya kusajili wanachama na hapa Dar alikuwa Makamu Mwenyekiti na mmoja wa watu waliokuja kujiunga nasi ni Pili Ndimaye ila tulimuambia asubiri kumaliza muda wake wa uongozi ndani ya CCM”, amesema Shingwe.
Ameongeza kuwa Ndimaye amesajiliwa Oktoba 19 na kupewa kadi namba 1000363 na muda wowote kuanzia sasa ataitisha mkutano rasmi na waandishi wa Habari kwa ajili ya kuzungumza mengi zaidi huku akieleza kuwa moja ya sababu zilizomuondoa ndani ya CCM ni pamoja na kutuhumiwa kushiriki kutengeneza migogoro ya ardhi Kwa kuwasaidia wavamizi kupata nguvu ya Serikali za mitaa katika kumiliki Ardhi.