Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania Profesa Hamis Malebo akiwa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa unaondelea New York ,Marekani.
*Ni ufafanuzi katika mkutano unaondelea katika Umoja wa Mataifa
Na Mwandishi Wetu,New York ,Marekani
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Tanzania, Prof. Hamisi Malebo amesema kuwa Tanzania haina ardhi ya Mababu ,Ardhi ya Makabila pamoja na ardhi ya kimila.
Akijibu taarifa ya Mwandishi katika mada ya “Watu wa Asili wanaohamishwa toka sehemu moja kwenda sehemu nyingine “Amesema Profesa Malebo na kuongeza taarifa iliyotolewa haijazingatia sheria za ndani za nchi jambo linalosababisha upotoshaji”
Profesa ameyasema hayo katika mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uunaendelea hadi jijini New York nchini Marekani.
Katika mkutano huo kulikuwa na Kikao cha Kamati ya tatu ya Masuala ya Watu wa Asili kilichofanyika 15 Oktoba 2024 wakati wa uchangiaji wa taarifa iliyosomwa na Mwandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Masuala na Haki za Watu wa Asili, Bw. José Francisco Calí Tzay, aliibua suala Tanzania kuhamishwa sehemu moja kwenda nyingine.
Prof. Malebo alisisitiza kuwa msimamo wa Serikali kuwa makabila yote Tanzania yana haki sawa mbele ya sheria na hakuna kabila lenye haki zaidi ya mengine.
Aidha amesema wakati akichambua jinsi Mwandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Masuala na Haki za Watu wa Asili, Bw. José Francisco Calí Tzay, alivyoelezea masuala ya ardhi na watu wa asili aliuelezea mkutano huo kuwa Mwandishi hakuzingatia uhuru wa Nchi Wanachama.
Prof. Malebo alihoji juu ya Mwandishi ni kwa nini anaripoti masuala ya umiliki wa ardhi huku akifumbia macho na kupuuza sheria za ndani za nchi husika.
Prof. Malebo alisisitiza msimamo wa serikali ya Tanzania kuwa nchi yetu haina ardhi ya mababu wala ardhi ya makabila au ardhi ya kimila.
Profesa Malebo alibainisha kuwa katika sheria za Tanzania hakuna ardhi ya mababu wala ardhi ya makabila au ardhi ya kimila na akataka Mwandishi na Jumuiya ya Kimataifa itambue kuwa masuala hayo hayamo katika mfumo wetu wa sheria.
Alifafanua pia kinachoendelea katika eneo la Ngorongoro ni kuhama kwa hiari kufuatia wananchi kuelimishwa na wao wenyewe kupewa nafasi ya kuridhia na kujiandikisha kwa hiari kwa wakazi wanaotaka kuhama kutoka katika eneo hilo ili kupisha uhifadhi.
Prof. Malebo aliukumbusha mkutano huo juu ya mfumo mkuu wa Ikolojia wa Serengeti-Mara, ambao ni mfumo pekee uliosalia wa kuhama wanyamapori na haupo katika eneo lingine duniani.
Katika Mkutano huo Prof. Malebo alisisitiza kwamba, Tanzania ina mikoa 31 ya kiutawala, ikijumuisha 26 ya Bara na Mitano ya Zanzibar na kulingana na Katiba na Sheria za nchi, kabila lolote Tanzania linaweza kuishi popote nchini.
Ailitolea mfano kabila la Wamasai ambao kwa sasa wapo na wanaishi katika mikoa 22 ambayo ni 71% ya mikoa yote nchini Tanzania, ambako wanaishi na kutekeleza maisha yao ya kifugaji na kitamaduni.
Amesema Sera ya sasa ya ardhi inatoa haki ya kupata na kumiliki ardhi popote nchini ikiwa na dhamana ya kikatiba ya raia wake kusafiri na kuishi kwa uhuru ndani ya nchi.
Amesema Sera hiyo imewafanya wananchi wa Tanzania kuishi kwa amani na kwa maelewano.
Prof. Malebo aliongeza kuwa suala la ardhi ya mababu au ardhi ya asili haitumiki kwetu na wala haihuusu Tanzania kutokana na ukweli wa sheria yetu nchi.
Prof. Malebo alihitimisha kwa kumhabarisha Mwandishi Maalum kuwa kuna msemo mmoja nchini Tanzania unaosema, ‘Kuona ni kuamini’ na akamhoji ni lini atatembelea Tanzania, ardhi ya Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro, na Zanzibar ambapo amemuhakikishia atakuta zaidi ya makabila 123 yanayoishi pamoja na kuishi kwa maelewano na amani.
Katika taarifa iliyotolewa na mwandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa Prof.Malebo amemtaka kutembelea Tanzania hapo ndipo atashuhudia hali halisi badala ya kutegemea uvumi na propaganda anazopelekewa ambazo hazina msingi wala ukweli.
Mkutano huo kwa Tanzania ulihudhuriwa Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi na Prisca Kasalama Msaidizi wa Afisa Kamati ya Tatu wote kutoka katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Marekani