Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameshiriki Mkutano wa 18 wa Maspika wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (The Bureau of EAC Speakers) uliofanyika leo, tarehe 13 Novemba 2024 katika Hoteli ya Emara Ole-Sereni, Nairobi, Kenya.
Mkutano huo umejadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha mchango wa Maspika katika kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwake. Masuala muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na ushirikiano wa karibu baina ya Mabunge ya Nchi Wanachama, uboreshaji wa sheria za kikanda na utatuzi wa changamoto zinazokumba jumuiya hiyo katika kufikia maendeleo endelevu.
Katika kikao hicho, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amekabidhi rasmi nafasi ya Uwenyekiti wa Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Spika wa Bunge la Kenya, Mhe. Dkt. Moses Wetang’ula. Tukio hili limeashiria hatua muhimu ya kuendeleza uongozi madhubuti na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama wa EAC.