Watumishi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Dodoma wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na upendo ili kuweza kutekeleza mpango kazi wa Taasisi.
Hayo yamesema na Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lomelo wakati wa mafunzo ya VVU/UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza yaliyofanyika Eneo la Michoro ya Miambani Kolo wilayani Kondoa.
“Tunafanya kazi kubwa za kuboresha barabara na tunapokea mrejesho mzuri toka kwa wananchi hivyo nawataka watumishi wote tufanye kazi kwa ushirikiano na upendo”.
Kuhusiana na mada walizofundishwa na wataalam wa afya alisema watumishi kama wazazi wanapaswa kuwalinda watoto wa kiume na wa kike ili wawe na maadili katika makuzi yao wakati wao wanaendelea kujenga nchini.
Naye, Muelimishaji Rika ambaye ni Meneja wa Wilaya ya Chamwino, Mhandisi Nelson Maganga alisema lengo kubwa la mwaka huu ni afya ya akili mahali pa kazi kwani afya ya akili ndiyo kitu pekee kinachomfanya mtumishi akafanikisha utendaji kazi vizuri na kupitia mafunzo waliyoyapata kila mtu amekiri kuelewa na itawasaidia kufanikiwa katika utendaji kazi wao kazini.
Wakati huo huo, Mratibu wa VVU/UKIMWI TARURA Mkoa ambaye pia ni Afisa Utumishi, Bi. Anna Baigana alisema utaratibu wa kupima afya ni utekelezaji wa mpango wa Taasisi hivyo ni nafasi nzuri kwa watumishi kupata elimu na kupima afya ili kulinda afya mahali pa kazi.
Aliongeza kusema kwamba katika mafunzo hayo wameongeza kitu kikubwa hususan upande wa kulinda watoto ana imani wameongeza kitu kikubwa hususan eneo la kuwapa nafasi watoto baada ya kazi kwani muda mwingi wanakuwa kazini na hivyo kama wazazi wanapaswa kuwapa ulinzi watoto katika familia zao.
TARURA Mkoa wa Dodoma umefanya mafunzo hayo ambapo watumishi wa ofisi ya mkoa na wilaya zake ikiwa ni kutekeleza mpango kazi wa Taasisi.
#Wapatiwa mafunzo kuhusu ulinzi kwa watoto
Kondoa