Wakazi wa Mji wa Geita mkoani Geita wakiwa katika moja ya vituo vya kuboreshea Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani humo kwaajili ya kuboresha taarifa zao na kujiandiskisha leo ikiwa ni siku ya mwisho ya zoezi hilo mkoani Geita. Zoezi hilo pia linafanyika mkoani Kagera na lilianza Agosti 5 hadi 11,2024.
Wakazi wa Mji wa Geita mkoani Geita wakiwa katika moja ya vituo vya kuboreshea Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani humo kwaajili ya kuboresha taarifa zao na kujiandiskisha leo ikiwa ni siku ya mwisho ya zoezi hilo mkoani Geita. Zoezi hilo pia linafanyika mkoani Kagera na lilianza Agosti 5 hadi 11,2024.
Na Mwandishi Wetu, Geita
Wananchi wengi wamejitokeza
kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura ambalo limekamilika leo tarehe 11 Agosti, 2024 mkoani
Geita baada ya kufanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 05 Agosti, 2024.
Mwandishi wetu ameshuhudia
uwepo wa wananchi wengi vituoni haswa vijana ambapo kwenye baadhi ya maeneo
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ililazimika kuongeza vifaa na watendaji.
Wakizungumzia mwenendo wa
zoezi hilo Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Geita Mji, Bw. Yefred Mnyenzi
na Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi. Sarah Yohana
wamesema wengi waliojitokeza ni vijana ambao wanajiandikisha kwa mara ya
kwanza.
“Kwa siku hawapungui wapiga kura 10,000 ambao
wamejitokeza, kati yao wapiga kura wapya ambao wengi ni vijana ni kama 8,000
kwa siku, kwa ujumla nawapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi,” amesema
Bw. Myenzi, Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Geita Mji.
Kwa upande wake, Afisa
Mwandikishaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi. Sarah Yohana amesema
“Wananchi wamejitokeza kwa wingi haswa vijana, maeneo yaliyokuwa na wananchi
wengi zaidi ni ya Katoro, Rwemgaza na Kiziba ambapo tumeongeza vifaa na
watendaji wa vituo, kwa mfano, Katoro tumeongeza BVR Kits 10 na Waandikishaji
na Waendesha Vifaa vya Bayometriki 20”.
Wakizungungumza kwa nyakati
tofauti wapiga kura waliojiandikisha na kuboresha taarifa zao wameishukuru INEC
kwa kuboresha huduma kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ambayo
imerahisisha zoezi hilo jambo ambalo limepunguza muda wa kujiandikisha na
kuboresha taarifa ambapo wameweza kupata kadi zao ndani ya dakika tatu hadi
tano.
“Kwa mara ya kwanza nimeweza kupata kadi yangu
hii ya mpiga kura, ambayo itaniwezesha kupiga kura kumchagua kiongozi wangu.
Nashukuru kwa teknolojia iliyowekwa nimeweza kutumia takribani dakika nne hadi
kupata kadi yangu ya mpiga kura,” amesema Angel Lema ambaye amefikisha miaka 18
mwaka huu.
Wananchio wakijiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Picha zote na INEC.