Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA)imewajengea uwezo Wanahabari Mikoa ya Nyanda za juu Kusini namna bora ya kuandika na kuzitumia vizuri kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.
Meneja Mawasiliano Kanda ya Nyanda za Juu kusini Boniphace Shoo amesema mada zilizojadiliwa ni pamoja na maudhui mtandaoni pia kanuni za utangazaji wakati wa uchaguzi.
Shoo amesema TCRA itaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwakumbusha Waandishi namna bora ya kuripoti habari za uchaguzi.
Vile vile Waandishi wa habari wamekumbushwa kuiheshimu Tume ya Taifa ya uchaguzi kwani ndiyo pekee yenye dhamana ya kutoa matokeo ya uchaguzi nchini.
Kwa upande wake Mhandisi Baluye Kadaya amewataka Waandishi kuweka mizania sawa pindi wanapofanya vipindi na wanasiasa.
Amesema baadhi ya vyombo vya Habari hutoa upendeleo kwa wanasiasa na kuonesha mapenzi yao yao kwa vyama hivyo pia amewasa watangazaji kuacha kuvaa sare za vyama pindi wanapofanya vipindi katika Vituo vyao.
Aidha Judith Nyange amesema TCRA imebaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa maudhui mtandaoni.
Katika hatua nyingine amewaasa Waandishi wa habari nchini kuendelea kujikumbisha mara kwa mara sheria na kanuni za uchaguzi.
Mchungaji Jacob Mwenga kutoka Makambako Njombe ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ameziomba Taasisi mbalimbali nchini kama Sensa,Tume ya Uchaguzi na TCRA kutoa elimu ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo Waandishi wa habari badala ya kufanya mafunzo kama matukio.
John Godfrey kutoka Mkoa wa Iringa amesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka hivyo watafanya kazi kwa uweledi mkubwa hasa namna ya kuandaa matangazo kipindi cha uchaguzi.
Godfrey Mwaifunga kutoka Njombe amesema TCRA semina hiyo itawezesha namna bora ya kuandika uchaguzi.
Verediana Matthias kutoka Mbeya amesema wao kama Waandishi wa habari elimu hiyo wataifikisha kwa jamii.
Zenodina Massawe kutoka Tunduma Wilaya ya Momba Mkoa wa Songwe amesema mafunzo yamewapa uwanda mpana wa kuzielewa sheria na kanuni mbalimbali za uandishi kipindi cha uchaguzi.
TCRA haitasita huchukua hatua kwa combo chochote kitakachokiuka maadili ya uandishi na utangazaji.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika mwishoni mwa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utafanyika mwaka kesho ambapo hivi sasa maboresho ya daftari la wapiga kura linaendelea nchini.