Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amekutana na wananchi wa Izumbwe II na Iwiji na kusikiliza kero zao ili kuendelea kuzitafutia ufumbuzi.
Wananchi wa kijij cha Izumbwe II risala yao iliyosomwa na afisa mtendaji wa kijiji Kambona Mwahalende, wameomba kutatuliwa kero zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji safi na ubovu wa barabara.
Wananchi hao pia wakitoa kero zao kwa Mbunge wa Mbeya vijijini, wamesema, wamesema barabara bado ni tatizo katani kwao ikiwemo barabara ya Sayuma hadi Ileya B kisha kutokea kijiji jirani cha Mwakasita ambayo wameomba iangaliwe licha ya kwamba daraja katika eneo lililokuwa korofi tayari lilishajengwa.
Hata hivyo wananchi hao wanaomba kumalizia usambazaji wa nishati ya umeme kwenye vitongoji ambavyo bado havijafikiwa ikiwemo shuleni ili wanafunzi wajisomee vizuri.
Akijibu hoja za miundombinu ya barabara Mhandisi Arcad Tesha ambaye ni Kaimu meneja wa Wakala wa barabara mjini na vijijini TARURA wilayani Mbeya amesema barabara inayolalamikiwa kutoka Sayuma kwenda hadi kijiji jirani cha Mwakasita haitambulikani hivyo wataifuatilia ili kuiingiza kwenye mpango wa bajeti.
Naye Mhandisi wa maji kutoka Wakala wa usambazaji maji vijijini RUWASA wilaya ya Mbeya Evetha Nzogela kwa niaba ya meneja wa RUWASA wilaya anasema wadau ambao ni shirika lisilo la kiserikali CRS limejitoa kujenga mradi wa maji katika moja ya vijiji vitatu vya kata ya Iwiji na endapo kijiji cha Izumbwe hakitanufaika RUWASA itahakikisha inakikumbuka kijiji hicho ili kumtua mama ndoo kichwani kwa kutafuta chanzo cha maji ili kujenga mradi kwa maslahi ya wananchi hao.
Mhandisi Nzogela amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki wakati wahisani hao wakiandaa mazingira ya kujenga mradi katani humo.
Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amewahakikishia wananchi kuwa kero zao zitaendelea kutatuliwa kama ambavyo baadhi zimeendelea kushughulikiwa.