Na Woinde Shizza, Arusha
Serikali imepiga kengele ya tahadhari kufuatia ongezeko la madai feki ya bima yanayodaiwa kuisababishia nchi hasara ya mabilioni, huku ikiweka wazi kuwa asilimia 10 hadi 15 ya madai hayo duniani yana chembechembe za udanganyifu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Sada Mkuya, amesema hali hiyo imeifanya sekta ya bima kupoteza uaminifu wa umma na kuathiri utoaji wa huduma kwa wateja wa kweli wanaohitaji msaada halali.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, wakati wa mkutano wa wataalamu wa udhibiti wa udanganyifu wa bima (IASIU), Dk. Sada alisema baadhi ya maofisa wa bima wanashirikiana na wateja kudanganya kwa malipo hewa, jambo alilolieleza kuwa ni uhujumu uchumi.
Fedha zinazopotea kwa njia ya hila hizi zingetumika kuboresha huduma kwa wananchi Serikali haiwezi kufumbia macho wizi huu unaotendeka kwa hila ya taaluma,” alisema na kupendekeza kuanzishwa kwa mahakama au kitengo maalum kitakachoshughulikia uhalifu wa bima kwa haraka na kwa haki.
Kamishna wa Bima nchini, Dk. Baghayo Saqware, alisema serikali tayari imeanzisha kitengo maalum cha kuchunguza udanganyifu wa bima, huku ikiimarisha miongozo na weledi wa wafanyakazi katika kampuni husika.
Amesema licha ya juhudi za kutoa elimu kwa umma, wahusika wa udanganyifu nao wameendelea kubuni mbinu mpya kila kukicha, hivyo mashirikiano ya kitaifa na kimataifa ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati wowote.
Rais wa IASIU Tanzania, Mjabwa Hanzuruni, aliitaka sekta binafsi kushirikiana na serikali kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na kuripoti madai yenye mashaka, akisema hatua hiyo itajenga uaminifu mpya katika soko la bima