Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza, ameendelea na ziara yake kwa mara nyingine baada ya kumalizika kwa vikao vya bunge akikutana na wananchi katika vijiji na kata mbalimbali ili kusikiliza kero zinazowakabili kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi na kukagua miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Mbunge Njeza ameendelea na ziara yake katika vijiji kadhaa vya kata za Iyunga Mapinduzi na Igale.
Akiwa katika kata ya Iyunga Mapinduzi amesikiliza kero za wananchi ambao kwa nyakati tofauti wameshukuru kwa namna miradi inayoendelea kutekelezwa ikiwemo usambazaji huduma ya umeme vijijini, usambazaji huduma ya maji na uboreshaji miundombinu ya elimu licha ya baadhi ya changamoto kuendelea kuwakabili.
Wananchi hao wameeleza kukabiliwa na kadhia ya bei kubwa ya huduma za afya hasa huduma ya upasuaji kwa akina mama.
“Sisi hapa tunamuomba mama yetu ni mwanamke kama sisi tunasikia anamwaga hela kwa Simba na Yanga basi atupunguzie bei za upasuaji na sisi huku maana hata mimi napenda Simba na Yanga”, ameeleza mwananchi wa kata ya Iyunga Mapinduzi Mwile Mboko.
Naye Rashid Fungambili mkazi wa kijiji cha Shuwa katani humo ameomba Serikali kupeleka daktari katika kijiji chao ambacho kina zahanati na kata ina kituo cha afya tarajiwa.
Mbunge Oran Njeza wa Mbeya vijijini, amepokea kero hizo kwa ajili ya kuziwasilisha kwa wataalam kuzitafutia ufumbuzi mara moja ambapo kuhusu huduma za afya kwa ujumla amewashauri wananchi wake kujiunga na bima ya afya kwa wote ili kupata matibabu hata wasipokuwa na fedha.
Amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya ikiwemo kujenga na kuboresha vituo vya afya kuwa vya kimkakati na kwenye kata hiyo amesema kituo cha afya cha kimkakati kitajengwa ili kuhudumia kata za Iyunga Mapinduzi, Isuto na Itawa.
Kero nyingine ni pamoja na barabara hasa kuelekea msimu wa mvua ambapo Mbunge huyo amewaondoa hofu wananchi kwa kumuinua afisa kutoka wakala wa barabara Tanzania TANROADS mkoa wa Mbeya ambaye amesema barabara ya Mbalizi Shigamba (Km 52) inaanza kujengwa Oktoba 2024.
Kuhusu barabara ya Iyunga Mapinduzi kwenda Shisonta afisa kutoka wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA Mhandisi Mollel ameipokea na kuahidi TARURA kuiingiza kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha (2025-2026) ili ijengwe kwa kiwango bora.
“Mheshimiwa Mbunge kuhusu barabara hii ya Iyunga Mapinduzi Shisonta naomba nichukue, tutaiingiza kwenye bajeti ya 2025-2026”, ameeleza Mhandisi Mollel.
Pamoja na hayo Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, ameendelea kuhimiza wananchi kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao shuleni ambapo katika kila shule aliyopita amechangia shilingi laki mbili ili kuwaunga mkono wananchi hao.