Mbeya, Agosti 2025 – Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya imetangaza kufanikisha uokoaji wa zaidi ya shilingi milioni 47 na kuziwezesha Halmashauri kuongeza mapato ya ndani kwa zaidi ya shilingi milioni 200 kupitia ufuatiliaji na udhibiti wa mianya ya rushwa na upotevu wa fedha za umma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Maghela P. Ndimbo, mafanikio hayo yametokana na kazi za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, uchambuzi wa mifumo ya ukusanyaji mapato, na kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2025.
Miradi ya Maendeleo na Huduma
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, TAKUKURU ilibaini ubadhirifu wa shilingi milioni 30 zilizotolewa kwa kikundi cha mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Fedha hizo zilielekezwa kwa matumizi mengine kinyume cha taratibu, lakini baada ya ufuatiliaji, kiasi hicho kilirejeshwa kikamilifu kwenye akaunti ya Halmashauri.
Vilevile, uchunguzi ulifanyika kwenye miradi 24 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 8.7 bilioni katika sekta za elimu, afya, barabara na miundombinu. Uchunguzi huo uliibua mapungufu ya utunzaji wa vifaa vya ujenzi na kusababisha upotevu wa mali, hatua zilizochukuliwa zikiwemo uchunguzi maalum na usimamizi zaidi.
Uboreshaji wa Mapato ya Halmashauri
Kupitia uchambuzi wa mifumo ya mapato, TAKUKURU Wilaya ya Mbarali iliwezesha Halmashauri kuongeza mapato kwa shilingi 214,337,401.2. Utafiti ulionyesha mianya ya rushwa katika ulipaji wa ushuru wa huduma, leseni za biashara na kodi za vibanda, ambapo baadhi ya wafanyabiashara walikuwa hawalipi ipasavyo kutokana na ukosefu wa ufuatiliaji.
FEDHA ZA MICHANGO YA WANAFUNZI
TAKUKURU imeokoa shilingi 17,023,750/= ambazo ni fedha za wanafunzi wa chuq ambao walizidisha katika kulipa ada stahiki kwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya – MUST.
- Ilibainika kuwa jumla ya wanafunzi 57 kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2025 walikua wakidai malipo ya fedha kiasi cha shilingi 17,023,750/= walizokuwa wamelipa zaidi kwenye akaunti ya chuo kipindi walipokuwa wanafunzi wa chuo
Baada ya kubaini hayo hatua zifuatazo zilichukuliwa;
- Kuitisha kikao vya majadiliano na Uongozi wa Chuo cha MUST na kuweka mikakati ya namna ya kulipa fedha za wanafunzi
- Hadi kufikia Juni 26, 2025 wanafunzi wote 57 walilipwa madai yao waliyokuwa wakikidai chuo
.
Uelimishaji na Mapambano Dhidi ya Rushwa
TAKUKURU iliendelea na programu za elimu kwa wananchi kupitia klabu za wapinga rushwa, semina 34, mikutano ya hadhara 36, vipindi vya redio 4 na makala mbalimbali. Pia ilitekeleza programu ya TAKUKURU-Rafiki kwa kushughulikia kero 63 kutoka kata 14.
Wito kwa Wananchi
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Maghela P. Ndimbo, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mmoja kwa manufaa ya Taifa.
👉 TAKUKURU inakumbusha wananchi wote:
Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu; tutimize wajibu wetu.