Mbeya. Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Eng. Kundo A. Mathew, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha miradi yote ya maji mkoani Mbeya na Chunya inakamilishwa kwanza kabla ya kuanzisha mingine, ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili, Mhe. Kundo alisema miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Maji Chunya inakidhi vigezo vya upatikanaji wa maji, wingi wa maji na gharama nafuu. Pia ameeleza kuwa chanzo cha maji kilibadilishwa baada ya visima awali kubainika kuwa na maji kidogo na chumvi nyingi, huku mazungumzo ya ufadhili na Serikali ya India yakiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, amesema miradi ya maji inaendelea licha ya changamoto za kifedha, akisisitiza kuwa sekta ya maji ni kipaumbele cha juu cha Serikali. “Wananchi wanatarajia huduma ya maji, na jitihada zinaendelea kuhakikisha miradi yote inakamilika kama ilivyopangwa,” alisema.
Akitoa taarifa ya utekelezaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya UWSA, CPA Gilbert Kayange, amesema Serikali imelipa zaidi ya Shilingi bilioni 26 kati ya Shilingi bilioni 31.7 za gharama za mradi, hatua iliyomwezesha mkandarasi kurejea site. Kazi muhimu zimeendelea, ikiwemo intake ya kuchukua maji, ujenzi wa bomba kuu, na tenki la kuhifadhi maji limefikia takribani asilimia 50. Aidha, zoezi la uthamini na fidia kwa wananchi limekamilika, likiwezesha mkandarasi kuendelea na kazi bila vikwazo.
Naibu Waziri alisisitiza kuwa Serikali haitaanzisha miradi mipya kabla ya kukamilisha ile iliyopo, ili matokeo ya huduma ya maji yafikie wananchi haraka. RC Malisa na CPA Kayange wamesema jitihada hizi zinahakikishia miradi inakamilika kwa ratiba na kwa manufaa ya wananchi.

