Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini imefanya matembezi ya amani leo, ikiwa ni sehemu ya ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya miaka 49 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi, kilichoasisiwa Februari 5 mwaka 1977.
Akizungumza mara baada ya matembezi hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Emmanuel Mwalupindi, amewataka wanachama wa chama hicho kuondoa hofu na uoga katika kukitumikia chama chao, akisisitiza kuwa CCM ni chama chenye misingi imara na historia kubwa ya kulihudumia Taifa.
Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Walimu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Daud Siame, ametumia nafasi hiyo kuhimiza amani, mshikamano na umoja miongoni mwa wanachama wa chama hicho, akisema mshikamano ndio nguzo muhimu ya mafanikio ya chama na Taifa kwa ujumla.

Baadhi ya wanachama walioshiriki katika matembezi hayo wameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na chama hicho, ikiwemo katika sekta za elimu, afya na miundombinu, wakisisitiza kuwa CCM imeendelea kugusa maisha ya wananchi.

Maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi yanaendelea nchi nzima kwa shughuli mbalimbali za kijamii, huku wanachama wakisisitiza umoja, amani na mshikamano kama msingi wa kuendeleza maendeleo ya Taifa.

