ASANTE MBEYA YAGUSA WAHITAJI IGURUSI MBARALI YATOA MAGODORO 46 KWA WAHITAJI.
Umoja wa Asante Mbeya Project unaoongozwa na Mkurugenzi wake Daniel Mwanakatwe(MC DANNY FM)umetoa magodoro arobaini na sita yenye thamani ya shilingi milioni mbili laki tano na elfu thelathini kwa watu wanaoshi mazingira hatarishi Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya hafla iliyofanyika Kijiji cha Lunwa Kata ya Igurusi Mgeni rasmi akiwa ni Mheshimiwa Diwani Hawa Kihwele.
Daniel Mwanakatwe ambaye ni Mkurugenzi wa Umoja huo amesema umoja wao una malengo matatu la kwanza kuwagusa Wahitaji pili kusaidiana wao na tatu kuwezeshana kiuchumi na kupeana fursa.
Amesema lengo la kutoa magodoro ni kuungana na Serikali kwa lengo la kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia unaofanywa na ndugu wa karibu pindi wanapowatembelea katika kaya zao.
“Godoro hili litamsaidia mtoto pindi wanapokuja wageni mtoto hatalala na ndugu badala yake mtoto atahamishwa peke yake ili mgeni alale peke yake lengo si kuvunja undugu bali ni kuweka ulinzi kwa watoto”alisema Mwanakatwe.
Mlezi wa Umoja huo Tumaini Mbembela ambaye pia ni muimbaji wa nyimbo za injili na mjumbe wa mkutano Mkuu Taifa kupitia Umoja wa Wanawake Mkoa wa Songwe amesema tendo lililofanyika ni sadaka mbele za Mungu.
Aidha Mbembela amewataka wadau wengine kuungana na Asante Mbeya ili kuwasaidia wahitaji kwani ni wengi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Igurusi Hawa Kihwele ameupongeza uongozi wa Asante Mbeya kwa ubunifu mkubwa wa kuwagusa wahitaji kwenye Kata yake.
Casmiri Pius ni Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Igurusi amesema msaada umekuja kwa wakati kwani wahitaji ni wengi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lunwa Isihaka Kimamule ameshukuru umoja wa Asante Mbeya kuwasaidia wananchi wake kwani wahitaji ni wengi.
Maclina Michael mkazi wa Lwanyo amesema yeye ni mmoja wa watu wanaoshi mazingira hatarishi amesema godoro alilopewa litaisadia familia yake.
Esther Mwaifuge Mkazi wa Chamoto amewashukuru wana Umoja wa Asante Mbeya kwa kuwajali watu wenye uhitaji.
Saita Mwanyingili bibi mwenye umri wa miaka tisini naye hakusita kuwashukuru wana Umoja wa Asante Mbeya kwa kuwafikiria watu wenye uhitaji kama yeye.
Lwitiko Minga amesema amesema binafsi asingeweza kununua godoro kutokana uchumi wake kuwa duni.
Umoja wa Asante Mbeya una wanachama nchi nzima na wanamiliki usafiri wao wa basi aina ya Coaster na wapo mbioni kununua usafiri mwingine ili kupanua wigo wa huduma na kuongeza kipato.