CPA. Gilbert Kayange, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya leo tarehe 16/11/2024 ametembea mtaa kwa mtaa kusikiliza na kutatua changamoto za wateja pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na Mamlaka.
Mkurugenzi Mtendaji ametembelea na kukagua mradi wa maji wa mto Simba, mradi wa kuboresha huduma ya maji kupitia visima virefu vya Gombe kusini na Mwasenkwa na mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Kata ya Iyunga.
CPA. Kayange amesema, Serikali inawekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi ili kuhakikisha kwamba Wananchi wanapata huduma bora na endelevu .
Aidha, katika ziara hiyo CPA. Kayange ameshuhudia miradi ambayo imefika hatua ya kuanza kuhudumia na kunufaisha wakazi wa maeneo mbalimbali. Mradi hiyo ni mradi wa kuboresha upatikani wa huduma ya maji Gombe Kusini na mradi wa mto Simba ambao unanufaisha Wananchi wa maeneo ya Mwasanga, Tembela, Ijombee na Sitoi.
Vile vile, Mkurugenzi Mtendaji amewaasa Wananchi kutoharibu miundombinu ya maji kwa kujifanyia maunganisho yasiyo halali na kuisababishia Taasisi hasara kupitia upotevu wa maji na kuathiri upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wengine.
Aidha, CPA. Kayange ametoa wito kwa Wananchi kulipa ankara za maji kwa wakati ili kuijengea Mamlaka uwezo wa kutoa huduma endelevu.