Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge Jimbo la Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wananchi wa Mbeya kuendelea kuiamini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amewataka Wananchi hao kushiriki kikamilifu kwa kuwachagua Viongozi wa CCM kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 11 Novemba, 2024 wakati akikabidhi nyumba za kuishi kwa Wananchi waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu Jijini humo. Waliokabidhiwa nyumba hizo ambazo zimejengwa na Taasisi yake ya Tulia Trust ni pamoja na Bi. Winifrida Kapingu mwenyeji wa Kata ya Ilemi, Bibi Tusekile Kazimoto na Bibi Mwaine Lumbalile wakazi wa Kata ya Iyunga.
Akizungumza na Wananchi hao, Dkt. Tulia amesema kuwa, Jiji la Mbeya limekuwa na changamoto nyingi na za muda mrefu ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, elimu, afya, maji n.k ambapo katika kipindi kifupi cha Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita tayari changamoto hizo kwa kiasi kikubwa zimepatiwa ufumbuzi.