Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Maryprisca Mahundi, ametimiza ahadi yake kwa wanawake wa Wilaya ya Kyela kwa kukabidhi mtambo wa kuchakata dhahabu (Karasha) kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani humo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mhe. Mahundi alisisitiza dhamira yake ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, akisema:
“Lazima tuhakikishe tunasimamia maono yetu. Mimi kama kiongozi, nina jukumu la kuhakikisha tunakua pamoja, hasa kundi kubwa la wanawake ambao nawaongoza.”
Aliongeza kuwa mtambo huo wa kuchakata dhahabu utasaidia kuinua uchumi wa wanawake wa Kyela kwa kuwaongezea fursa za kipato na maendeleo endelevu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Kyela, Bi Sesilia Mwakang’ata, alimpongeza Naibu Waziri Mahundi kwa juhudi zake za kuleta maendeleo kwa wanawake wa Mbeya.
“Tunamshukuru sana kwa kutupatia mradi huu wa kuchakata dhahabu. Ni hatua kubwa katika kutufanikisha kiuchumi na tunaupokea kwa mikono miwili,” alisema Bi Sesilia.
Mradi huu unatarajiwa kuongeza fursa za ajira kwa wanawake wa Kyela na kuboresha hali yao ya kiuchumi kupitia sekta ya madini.