WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa zaidi ya wakulima 18,000 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na Mpango wa Taifa wa Kilimomisitu ifikapo mwaka 2031, ambao unalenga kuhakikisha wakulima milioni 15 wanatumia teknolojia na mbinu bora za kilimomisitu nchini.
Mkakati huo uliozinduliwa mwaka 2024 na Mhe Dkt. Philipo Isdori Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umejikita katika kuendeleza kilimomisitu nchini, ikiwa na dhima ya kukuza ufanisi wa mbinu za kilimomisitu na teknolojia zake ili ziweze kutumika na jamii ya wakulima kwa ajili ya kudumisha ustawi wa jamii, uchumi na mazingira.
Akizungumza leo Agosti 6, 2025 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya Kilimomisitu, Waziri Chana alisema kuwa Mkakati huo uliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na unalenga kukuza ufanisi wa matumizi ya teknolojia za kilimomisitu ili ziweze kutumiwa na jamii ya wakulima katika kuboresha ustawi wa jamii, uchumi na mazingira.
“Ili kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huu unafanyika kwa ufanisi, Wizara imeunda Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ambayo leo naizindua rasmi. Kamati hii itakuwa na jukumu la kushauri na kusimamia utekelezaji wa mkakati huu,” amesema Waziri Chana.
Alifafanua kuwa Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo la nchi kavu, ambapo asilimia 93 ni misitu ya uoto wa Miombo na asilimia 7 ni misitu ya Uwanda wa Chini, Milimani, Mikoko na mashamba ya miti.
Hata hivyo, alionya kuwa misitu inakabiliwa na changamoto kubwa kama uvamizi, uchomaji mkaa, moto wa misituni na uchimbaji haramu wa madini. “Takwimu zinaonesha kuwa hekta 469,400 za misitu hupotea kila mwaka. Kiwango hiki ni kikubwa mno na kinapaswa kudhibitiwa,” alisisitiza.
Alibainisha kuwa wakulima ni wadau muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Kilimomisitu kutokana na nafasi yao katika kilimo na uhifadhi wa mazingira, hivyo wataunganishwa katika minyororo ya thamani ya bidhaa za kilimomisitu ili kuongeza kipato na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Misitu, Bw. Daniel Pancras, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, alisema kuwa Kamati hiyo inaundwa na wajumbe tisa kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, TFS, TAFORI, TARI-Tumbi, SHIWAKUTA, Bodi ya Kahawa na Vi-Agroforestry.
Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo alisema kuwa kilimomisitu ni mbinu shirikishi ya kuchanganya miti na mazao ya chakula ili kuongeza uzalishaji, kuhifadhi mazingira na kusaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Mkakati huu utawezesha upatikanaji wa mbegu na miche bora, kuimarisha uwezo wa kitaifa kusimamia mifumo ya kilimo mseto, kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko na kuchochea urejeshaji wa ardhi na uhakika wa chakula,” alisema Prof. Silayo.
Alisema kuwa mafanikio ya mkakati huo yatategemea ushirikiano wa wadau wote katika sekta za misitu na kilimo, na kuhimiza matumizi ya maarifa ya kisasa katika kilimo mseto ili kulinda mazingira na kukuza maendeleo endelevu.