Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la CARE wametoa mafunzo kwa wawezeshaji wa ngazi ya jamii kuhusu mabadiliko ya tabia nchi katika mkoa wa Mbeya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu.
Mradi huo unatekelezwa katika vijiji 300 vya mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa kwa lengo la kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuboresha utunzaji wa mazingira.
Katika mkoa wa Mbeya, mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tatu wilayani Mbarali, kijiji cha Chimala, yakilenga zaidi wakulima na wafugaji ili kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya jinsia, uhifadhi wa mazingira na mbinu za kuielimisha jamii juu ya mabadiliko ya tabia nchi. TGNP na CARE wameeleza kuwa wataendelea kutoa elimu katika vijiji vyote vinavyonufaika na mradi huo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kubainika kwa changamoto ya upungufu wa maji inayochochea migogoro kati ya wakulima na wafugaji, huku wanawake, vijana na makundi maalum wakiwa miongoni mwa waathirika wakubwa.
Aidha, kupungua kwa mvua kumesababisha wakulima kukosa mavuno na wafugaji kukabiliwa na uhaba wa malisho, hali inayochangia vifo vya mifugo pamoja na kushuka kwa thamani yake.
Mkufunzi kutoka TGNP, Rose Ngunangwa, amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa mafunzo kwa jamii mbalimbali chini ya mradi huo ili kuongeza uelewa na kuchochea ushiriki wa wananchi katika kulinda
mazingira.
Baadhi ya wawezeshaji walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa ukame unaotokana na ukosefu wa elimu ya utunzaji wa mazingira umeathiri kwa kiwango kikubwa shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wake, Rubeni Mwale, mkazi wa kijiji cha Kamwale na mmoja wa washiriki, amesema mafunzo hayo yamewapa uelewa mpya na yatawasaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kueneza elimu kuhusu athari na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kupitia mpango huo, TGNP na CARE Tanzania wanaendelea kuiwezesha jamii kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya maendeleo endelevu.

