Mfumo wa kidigitali wa utoaji wa Vyeti vya Uasili kupitia Tanzania Chamber Portal (TCP) unaopatikana kupitia tovuti ya tcp.tncc.or.tz unatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia Machi 2, 2026, hatua inayolenga kurahisisha na kuharakisha huduma za biashara za kimataifa nchini.
Akizungumza mkoani Mbeya wakati wa mafunzo kwa wasafirishaji wa bidhaa kwenda nje (exporters), Makamu wa Rais Kilimo wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Bw. Swallah Swallah, amewahimiza wafanyabiashara kujiandaa na kuutumia kikamilifu mfumo huo kwa kujisajili na kuwasilisha maombi yao kupitia tcp.tncc.or.tz, ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku.
Alisema kuanza kwa kutumika kwa mfumo huo wa kidigitali wa utoaji wa Vyeti vya Uasili (Certificate of Origin) kupitia Tanzania Chamber Portal (TCP) ni hatua muhimu itakayoongeza uwazi, kasi na ufanisi katika mchakato wa kupata nyaraka muhimu za biashara za kimataifa kwa njia ya mtandao.
“Kuanzia Machi 2, 2026, tunafungua ukurasa mpya wa utoaji wa Vyeti vya Uasili kwa njia ya kidigitali kupitia tcp.tncc.or.tz.
Mfumo huu utaondoa urasimu, kupunguza muda wa kusubiri na kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wetu katika masoko ya nje,” alisema Bw. Swallah.
Alifafanua kuwa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na TNCC yamefanyika katika mikoa 14 ikiwemo Mbeya, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Songwe, Dodoma, Iringa, Njombe, Morogoro, Lindi, Mtwara, Singida, Kigoma na Tabora, kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi wa Chemba na wafanyabiashara ili waweze kutumia mfumo huo kwa ufanisi tangu siku ya kwanza ya utekelezaji wake.
Kwa upande wake, mfanyabiashara anayesafirisha mahindi na mchele nje ya nchi, Bi. Felister Mutalemwa, alisema mfumo huo utapunguza gharama na muda wa kushughulikia nyaraka za usafirishaji kwa kuwa huduma zote zitapatikana mtandaoni kupitia tcp.tncc.or.tz.
“Kwetu sisi tunaosafirisha mazao ya kilimo, mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa Vyeti vya Uasili bila kulazimika kufuatilia kwa muda mrefu au kusafiri umbali mrefu.
Hii itaongeza ushindani wetu katika masoko ya nje na kupunguza ucheleweshaji wa mizigo,” alisema Bi. Mutalemwa.
Alitoa wito kwa Serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya kidigitali na kuhakikisha inawafikia wafanyabiashara wa maeneo yote ya nchi, huku akiwahimiza wafanyabiashara wengine kujitokeza kujifunza, kujisajili na kutumia mfumo huo kikamilifu kupitia tovuti hiyo.
Warsha hiyo inafanyika kwa udhamini wa TradeMark Africa kwa kushirikiana na Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa na mazingira bora na rafiki kwa biashara za kikanda na kimataifa.

