Author: Mbeya Yetu

Mbeya. Watu 11 wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea leo Septemba 27 wilayani Mbeya mkoani hapa.

Ajali hiyo imetokea eneo la Jojo Kata ya Ilembo wilayani humo ikihusisha gari aina ya Fuso ambayo ilikiwa ikielekea kwenye soko kwa ajili ya mnada.

Mmoja wa mashuhuda katika eneo hilo, Elias Shiwiwi amesema gari hilo kampuni ya Chakazi likiwa limebeba wafanyabiashara kwa ajili ya mnada wa leo, lilikatika propela na kusababisha vifo kadhaa.

“Palepale wamefariki watano, baadaye wengine watano wakafia njiani wakielekea kituo cha afya Ilembo nikiwa naona hadi kufika kituoni hapo” amesema Shiwiwi.

Mganga mkuu wa kituo cha Afya Ilembo, Dk Philimon Irungi amethibitisha kupokea miili ya watu 11 ambapo mwingine mmoja alifariki baada ya kufika kituoni hapo.

“Eneo la tukio walifariki 11, ikatangulia miili sita kisha ikaja mitano na mmoja akafariki wakati akipatiwa matibabu, majeruhi ni 21” amesema Dk Urungi.

Read More