Author: Mbeya Yetu

*DKT. TULIA ATOA SOMO KWENYE MKUTANO WA MABUNGE YA SADC*

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amewaasa Wabunge wa Jukwaa la Mabunge ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC) kuwa mstari wa mbele kuhakikisha nchi zao zinatoa kipaumbele katika upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi wengi zaidi.

Mhe. Spika ameyasema hayo wakati akichangia Mada kuhusu mwelekeo wa upatikanaji wa nishati ya uhakika, endelevu na inayojitosheleza katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika kwenye wa Mkutano wa 51 wa Jukwaa la Mabunge ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC – PF) unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Bingu Lilongwe nchini Malawi.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali za nchi wanachama zinapaswa kuzingatia uhalisia wa vyanzo vya upatikanaji wa nishati ya umeme katika nchi husika ili kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa nishati hiyo katika eneo la kusini mwa Afrika.

“Kama nchi nyingi za SADC bado zipo gizani, ni muhimu kutafuta suluhisho la upatikanaji wa nishati ya umeme kwa kutumia vyanzo vilivyopo ili kuwaondolea wananchi wetu changamoto hiyo.” Alisema Dkt. Tulia

Mhe. Dkt. Tulia aliainisha baadhi ya mikakati ya Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme kuwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwl. Nyerere linalotarajiwa kuzalisha takribani Megawati 2100 pamoja na mradi wa ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asilia kwenye kina kiferu cha bahari mkoani Lindi.

Katika Mkutano huo, Mhe. Spika ameambatana na Wajumbe wa Jukwaa hilo kutoka Bunge la Tanzania ambao ni Mhe. Selemani Zedi, Mhe. Shally Raymond, Mhe.Hawa Mwaifunga, Mhe. Dkt. Alfred Kimea na Mhe. Haji Kassim.

Read More