Browsing: Video Mpya

Mkazi wa eneo la Soweto, jijini Mbeya, Rashidi Mkwinda, ambaye ni mwandishi wa habari wa Mbeya Yetu Online TV, amesimulia tukio la kuvamiwa na kupigwa kichwani na watu wanaodhaniwa kuwa vibaka majira ya saa sita usiku.

Amesema alikuwa akirejea nyumbani baada ya kudownload faili kwenye kompyuta, ndipo alipofuatwa na watu hao na kushambuliwa wakati akifungua geti la nyumba yake. Katika tukio hilo alipigwa mara kadhaa kichwani, akaanguka chini na kupoteza fahamu kwa muda, kisha kuibiwa simu ya mkononi pamoja na fedha.

Baada ya kupata msaada kutoka kwa majirani, alikimbizwa hospitalini ambako alishonwa majeraha sehemu mbalimbali za mwili na kufanyiwa kipimo cha CT Scan, huku majibu yakitarajiwa kutoka leo.

Mkwinda ametoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya kihalifu vinavyoendelea kushamiri mitaani.

Kijana dereva wa bodaboda Brown Anthony amevunja rekodi baada ya kusafiri kutoka Mbeya hadi Dar es Salaam kwa saa 10 tu akitumia pikipiki aina ya Boxer 150 HD (MC 473 FKT).

Safari hii ilianza kama ubishani wa kawaida kati yake na bodaboda mwenzake Alex Ndile tarehe 14 Januari 2026, wakibishana kama inawezekana kufika Dar ndani ya masaa 13. Ubishi ukawekwa kwenye makubaliano rasmi, na Brown akaamua kuthibitisha kwa vitendo.

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, ameanza kutatua kero ya barabara katika Kata ya Iyela, mitaa ya Iyela na Pambogo, kwa kuagiza kumwagwa kwa vifusi kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya wakazi wa maeneo hayo. Hatua hiyo inalenga kuboresha hali ya barabara na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi za wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge, Katibu wa Mbunge Hakimu Edward alisema zoezi la kumwaga vifusi ni utekelezaji wa maelekezo ya moja kwa moja ya Mbunge Mwalunenge, ikiwa ni sehemu ya ahadi zake za kisiasa na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa vitendo.

Wananchi wa Kata ya Iyela, Jijini Mbeya, wameiomba Serikali kuangalia kwa jicho la huruma barabara ya eneo la Hali ya Hewa hadi Kituo cha Afya Iyela, wakieleza kuwa barabara hiyo imekuwa katika hali mbaya kwa zaidi ya miaka kumi. Wamesema barabara imejaa mashimo makubwa yanayosababisha vyombo vya usafiri ikiwemo bajaji na pikipiki kushindwa kupita kwa urahisi, hali inayowaathiri wananchi hususan wagonjwa wanaoelekea kupata huduma za afya katika kituo hicho.