Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar utafanyika
tarehe 08 Juni, 2024.
Taarifa
kwa umma iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Bw.
Kailima, R. K jijini Dodoma leo tarehe 02 Mei, 2024 imesema kwamba fomu za
uteuzi kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo zitatolewa kuanzia tarehe 17 hadi 23 Mei,
2024.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 23 Mei, 2024 na
kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo zitafanyika kuanzia tarehe 24 Mei, 2024 hadi
tarehe 07 Juni, 2024.
Tume
imetangaza uchaguzi huo mdogo kufuatia taarifa ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, iliyomtaarifu Mwenyekiti wa Tume kuhusu uwepo wa nafasi
wazi ya ubunge katika Jimbo la Kwahani.
Spika
ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 49(2) cha Sheria ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka, 2024.
“Kwa
kuzingatia matakwa ya kifungu cha 49(1)(b) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume inatoa taarifa kwa umma kuhusu
uwepo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya
Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Tume
imevikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba,
sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume
katika kipindi cha uchaguzi huo mdogo.