RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, amekiri kuvutiwa na mchango mkubwa wa Benki ya NMB wa Sh. Bilioni 1 kati ya Sh. Bil. 2.71 zilizokusanywa wakati wa hafla ya kuchangisha fedha za matibabu ya watoto 1,500, wanaotibiwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Dk. Kikwete alitoa pongezi hizo wakati wa hafla hiyo iliyoandaliwa na JKCI kwa kushirikiana na Heart Team Africa Foundation (HTAF), kupitia kaulimbiu: Tia Nuru, Gusa Moyo, Toa Matumaini kwa Maisha ya Watoto, lengo likiwa ni kukusanya fedha za matibabu ya watoto wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kikwete alisema Sh. Bil. 1 zilizotolewa na NMB, iliyosaini makubaliano ya ushirikiano na JKCI ya kutoa kiasi hicho kwa miaka minne, kinaenda kuiongezea nguvu Serikali inayopambania uamuzi wake wa kisera wa kuendelea kujenga uwezo wa ndani wa kutibu maradhi ya moyo.
“Gharama za kupeleka wagonjwa nje ni kubwa sana na huu ulikuwa ndio msukumo uliozaa uanzishwaji wa JKCI, leo taasisi imefikia hatua kubwa na bora katika matibabu ya moyo, ambako Serikali inagharamia asilimia 70 ya matibabu na familia kuachiwa asilimia 30 (saw ana Sh. Mil. 4), ambayo pia ni kubwa kwa walio wengi.
“Nimevutiwa na michango ya wadau wa afya, kipekee sana kwa mchango wa NMB. Pesa alizochangia dada’angu Ruth Zaipuna (Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB), ni nyingi mno, Sh. Bil. 1 waliyoitoa inaenda kuokoa maisha ya takribani watoto 250 kati ya 1,500 wakiwemo 500 wanaohitaji operesheni ya haraka,” alisema Kikwete.
Kikwete alizipongeza Serikali za Awamu ya Tano na Sita kwa kuendelea kuwekeza katika shughuli za Taasisi ya JKCI na kugharamia asilimia 70 za gharama za matibabu, ambapo taasisi imeendelea kuimarishwa kwa vifaa vya kisasa, huku akiwataka wadau zaidi kuendelea kusapoti jitihada za Serikali.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya Sh. Bil. 1, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Zaipuna alimpongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa maono yake yaliyolenga kutatua changamoto za Watanzania wanaosumbuliwa na Magonjwa ya Moyo na kuanzisha JKCI.
@nmbtanzania @taasisiyamoyo_jkci