Halmashauri ya Jiji la Mbeya imezitaka kampuni ya ujenzi ya Cico inayojenga jengo na barabara za mradi wa Tactic na Kampuni ya Mhandisi ambayo ni mkandarasi mshauri kwenye miradi hiyo kuwaondoa wasimamizi wake kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza baada ya ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za Kalobe-Itende, Machinjioni- Mapelele, Kabwe-Sido na Iziwa, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mhe.Dormohamed Issa amesema, hajaridhishwa na anapata wasiwasi na kasi ya maendeleo ya mradi na hana uhakika kama mkandarasi atamaliza mradi kwa wakati uliopangwa kwa mujibu wa mkataba.
Mstahiki Meya ameongeza kuwa tangu mkandarasi wa kampuni ya Cico alipokabidhiwa na kuanza kazi Novemba, 2023 hakuna alichokifanya kwenye barabara zote, hali ambayo inasababisha wananchi kuendelea kukabiliwa na changamoto ya barabara wakati Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, imeshatoa fedha, hivyo amemtaka mkandarasi kumuondoa Meneja Mradi Mhandisi Bw.Penfeng Wang na Kampuni ya Mhandisi ambayo ni Mkandarasi Mshauri, Bw.Jofrey Kanjanja kwa kushindwa kusimamia kasi ya mradi kama ilivyopangwa.