23 Mei 2024, jijini Tartu nchini Estonia, Mheshimiwa Injinia Maryprisca Mahundi, Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA, alifanya kikao na uongozi wa Taasisi isiyo ya kibiashara ya e-Governance Academy (eGA) ya serikali ya Estonia. Mkutano huo ulifanyika kandokando mwa Kongamano la 10 la Utawala wa Mtandao (10th e-Governance Conference) ambalo lilibeba kauli mbiu ya “Unlocking Digital Success”.
eGA ni kituo cha umahiri kilichojikita kwenye mapinduzi ya kidijitali ya jamii ndani ya Estonia na duniani kote. Kituo hicho kinawakutanisha wataalamu wabobezi mbalimbali wenye weledi wa mambo ya kidijitali kutoka Estonia. Katika kikao hicho, eGA iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti wa Bodi ya eGA, Mr. Hannes Aston, Mkuu wa Utawala na Mawasiliano, Ms. Marit Lani, na Mtaalamu wa Mahusiano na Wateja, Mr. Ants Urvak.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mheshimiwa Injinia Maryprisca Mahundi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dr. Nkundwe Mwasaga, na Ms. Joyce Malipula kutoka Ubalozi wa Tanzania Uswidi.
Mazungumzo ya kikao hicho yaligusa maeneo ya ushirikiano kati ya Estonia na Tanzania katika maeneo yaliyoainishwa kwenye tafiti iliyozinduliwa mwezi Oktoba 2023 kwenye Kongamano la TAIC jijini Dar es Salaam. Utafiti huo ulifanywa na eGA ya Estonia na Tume ya TEHAMA ya Tanzania na uliainisha njia ambayo Tanzania inatakiwa kupitia ili kuharakisha mapinduzi ya kidijitali (Roadmap to Digital Transformation of Tanzania).
Pande zote mbili zilikubaliana kuanzisha mchakato wa kufanyia kazi mambo yote yalioainishwa kwenye utafiti huo. Moja ya maeneo muhimu yaliyojadiliwa ni mfumo wa taarifa binafsi wa wananchi wa Tanzania (Data Protection Citizen Portal).