Kambi ya macho maalum kwa ajili ya wagonjwa wa mtoto wa jicho iliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya imepata mafanikio makubwa kwa wagonjwa waliofika Hospitalini hapo kuipongeza serikali na Shirika la Hellen Keller International kufanikisha matibabu bure.
John Mpozayo(73) mkazi wa Saza Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe ni mmoja wa watu waliokuwa wanasumbuliwa na mtoto wa jicho kwa macho yote mawili kwa miaka mitano naye hakusita kufika Hospitalini hapo ili kupatiwa matibabu.
Amesema alikuwa akipata changamoto mbalimbali kutokana na kadhia ya kutoona kwani mara nyingine alishindwa kwenda Kanisani na maeneo mengine hata kwenda maliwato alikuwa akiongozwa na mkewe hivyo kitendo cha yeye kupona kutamsaidia mkewe pia kufanya shughuli nyingine.
“Nimekwenda katika hospitali mbalimbali ikiwemo hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya pia Dar Es Salaam lakini sikufanikiwa licha ya kutumia gharama kubwa za usafiri na malazi ambapo mara zote nimekuwa nasafiri na mke wangu”alisema Mpozayo.
Baada ya kufanyiwa upasuaji Mzee Mpozayo ameonekana mwenye furaha huku akirukaruka akiishukuru serikali kwa kuliruhusu Shirika la Hellen Keller International kutoa matibabu kwa wagonjwa hasa wanaotoka pembezoni ambao hawawezi kumudu gharama za usafiri na matibabu.
Ameiomba serikali na Shirika la Hellen Keller International kuifanya huduma hiyo kuwa endelevu kwani wahitaji ni wengi na hawana uwezo wa kugharamia matibabu.
Kwa upande wake Christina Asukenie mke wa Mzee John Mpozayo mbali ya kufurahia matibabu ya mumewe amesema wamepata mkwamo kiuchumi kwani wametumia pesa nyingi kwa ajili ya kutafuta matibabu nje ya Mkoa wa Songwe.
“Kuna wakati tumesafiri kwenda kupatiwa matibabu ya macho katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya lakini kutokana na shinikizo la macho ya mume wangu alishindwa kufanyiwa upasuaji hali iliyoninyong’onyesha sana pamoja na watoto ambao walikuwa wakisaidia matibabu”alisema Christina huku akibubujika machozi ya furaha.
Shirika la Hellen Keller International hufanya uchunguzi wa awali kwa kutumia Madaktari bingwa wakiongozwa na watoa huduma ya afya ngazi ya jamii na wanaothibitika kuwa na changamoto ya mtoto wa jicho hufikishwa kwenye kambi maalumu iliyoandaliwa na Kambi ya Chunya ni ya kwanza kufanyika katika Wilaya hiyo nay a saba tangu Hellen Keller International kuanza kutoa huduma katika Mikoa ya Mbeya,Njombe na Songwe.