Anastazia Timotheo Kasela (26) mkazi wa Makongolosi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya ni mwanamke aliyezaliwa na ulemavu wa macho amelishukuru Shirika la Hellen Keller International kwa kufanikisha matibabu ya mtoto wa jicho yaliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
Anastazia aliyejaliwa kuwa na familia ya watoto wawili hakuwahi kuwatambua kwa sura zao wala hajui sura ya mumewe bali aliweza kuitambua sauti yake tu.
Katika Kambi hiyo ya mtoto wa jicho iliyoanza juni 19,2024 na kutamatika juni 24,2024 Anastazia ni miongoni mwa wagonjwa waliofika Hospitalini hapo akiwa hana matumaini lakini siku moja baada ya kufanyiwa upasuaji na kufunguliwa macho alijikuta mwenye furaha baada ya kufanikiwa kuona kwa mara ya kwanza tangu azaliwe.
“Nimefurahi kuona sura ya mtoto wangu kwa mara ya kwanza na pia nitafurahi kuona sura ya mume wangu nikirudi nyumbani”alisikika Anastazia huku akionesha tabasamu.