HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA MBEYA YAENDELEA KUWA KITUO CHA MFANO KATIKA USIMAMIZI WA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Katika jitihada za kuendelea kuboresha huduma chini ya Wizara ya afya nchini, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya imeendelea kuwa miongoni mwa vituo vya mfano katika umahiri wa usimamizi wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kupitia mpango maalumu wa usimamizi wa utoaji wa huduma bora katika maeneo ya kazi ujulikanao kama (5S – KAIZEN).
Akiongea baada ya kupokea ujumbe wa wataalam kutoka Wizara ya Afya ulioambatana na Viongozi kutoka nchi mbalimbali waliofika hospitalini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji amesema lengo kubwa la ugeni huo ni kujifunza na kujionea mpango maalum wa usimamizi wa utoaji wa huduma bora za afya ujulikanao kama (5S – KAIZEN) unatekelezwa na kusimamiwa na kitengo cha Ubora Hospitalini hapa.
“…tumepokea wageni kutoka Wizara ya Afya ya nchi ya Zimbabwe waliokuja hospitalini hapa kujifunza masuala yote yanayohusiana na ubora wa huduma na namna ya kuboresha mambo mbalimbali katika Hospitali.” – Dkt. Godlove Mbwanji
Aidha Dkt. Mbwanji amesema kama hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya wamejipanga kuendelea kuboresha huduma kupitia mpango huo, na kutoa wito kwa nchi mbalimbali kuendelea kutembelea hospitalini hapa kujifunza hasa masuala ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi kupitia mpango huo wa (5S – KAIZEN)
“…tumejipanga kuhakikisha tunaboresha utoaji wa huduma na tunatoa wito kwa nchi mbalimbali kuendelea kuja kujifunza masuala ya ubora na huduma kwa ujumla.” – Dkt. Godlove Mbwanji
Kwa upande wake mratibu ubora wa huduma kutoka Wizara ya Afya nchini Dkt. Anjelina Sijaona amesema kupitia mpango huo maalumu wa usimamizi wa utoaji wa huduma bora chini ya mradi wa “JAICA” nchini wamepewa nafasi ya kuwa kituo cha mfano wa kutoa mafunzo ya jinsi ya kutumia falsafa ya matumizi ya mpango maalumu wa kuboresha huduma wa “5s – KAIZEN”
“…tumepewa nafasi ya kuwa nchi ya kuonyesha umahili wa jinsi ya kutumia falsafa ya “5S – KAIZEN” katika kuboresha huduma kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu na kufanikiwa kupokea zaidi ya mataifa 7 kwaajili ya kujifunza.” – Dkt. Anjelina Sijaona
Dkt. Musiwarwo Chilume ni Mkurugenzi wa uhakiki ubora na usalama wa mteja Wizara ya Afya Zimbabwe amesema, wao kama ujumbe wa wataalamu wa afya kutoka Zimbabwe wamejifunza mambo mengi ikiwemo mifumo na falsafa ya usimamizi wa utaoji wa huduma bora za afya kitu ambacho kimepelekea uwepo wa usimamizi mzuri wa majukumu na uongozi bora ndani ya hospitali hii.
“… tumefurahi kwa kipindi tulichukuwepo hapa kwa kuwa tumejifunza mambo mengi chini ya utelekelezaji wa mpango huu wa “5s KAIZEN” hospitalini hapa uliopelekea uboreshaji wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.” – Dkt. Musiwarwo Chilume