Serikali imesema uanzishwaji maeneo ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) sura ya 287 na (Mamlaka za Miji) sura ya 288 pamoja na mwongozo wa uanzishwaji wa maeneo ya Utawala wa mwaka 2014.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Zainab Katimba, alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini Mhe. Oran Njeza aliyeuliza ni lini Serikali itarekebisha mipaka ya vijiji vya Kata ya Utengule Usongwe ikiwemo Kijiji cha Mbalizi ambacho hakiungani kabisa na Vijiji vingine.
“Kwa kuzingatia sheria hizi na mwongozo uliyopo, utaratibu wa uanzishaji au mabadiliko ya mipaka ya vijiji inapaswa kuanza kujadiliwa kwenye mkutano mkuu wa kijiji, kamati ya maendeleo ya kata (WDC), baraza la madiwani, kamati ya ushauri ya wilaya (DCC) na kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ambayo huwasilisha mapendekezo hayo Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia Katibu Tawala Mkoa”, amesema Katimba.
Naibu Waziri huyo amesema ni vema Halmashauri na Mkoa kufuata taratibu hizo na ombi hilo liwasilishwe Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kupitia Katibu Tawala Mkoa kwa hatua zaidi.