Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, imempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kwa Uongozi wake mahiri na ujasiri aliouonesha katika tukio lililotokea wakati wa Mkutano wa 149 wa IPU uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu mjini Geneva, Uswisi.
Mhe. Majaliwa amesema, “Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia ushupavu aliouonesha wakati wa Mkutano huo na jinsi alivyodumisha msimamo thabiti wakati wote. Sina shaka kuwa Uongozi wake utaacha alama ya kudumu katika historia ya Umoja wa Mabunge Duniani.”
Aidha, Mhe. Majaliwa amewaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono Mhe. Spika ili aweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. “Sote kwa pamoja, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu amjalie uzima, hekima na nguvu katika kuutumikia Umoja huo duniani,” amesisitiza Mhe. Majaliwa.