Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga barabara, vivuko na madaraja katika maeneo mbalimbali mkoani Katavi ili kuinua shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Japhet Bengesi alisema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuimarisha miundombinu ya barabara mkoani Katavi.
Mhandisi Japhet amemshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya TARURA mkoa wa Katavi kutoka Shilingi Bilioni 4 hadi kufikia Shilingi Bilioni 15 ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha mtandao wa barabara mkoani humo.
“Tumeweza kufungua barabara mpya ambazo hazikuwepo kabisa zenye urefu wa Km 439, barabara za changarawe zimeongezeka kutoka Km 471 hadi Km 692 ambalo ni ongezeko la Km 221 na barabara za lami kutoka Km 36 mpaka Km 53 ambalo ni ongezeko la Km 17 ndani ya miaka mitatu ambapo ni mafanikio makubwa”, alibainisha.
“Barabara za lami zimejengwa katika maeneo ya mijini na katika huduma za kijamii kama vile hospitali za wilaya ambapo katika wilaya ya Tanganyika tumejenga Km 1 ya lami ambayo imegharimu shilingi milioni 500”, alisema.
Aidha, alisema kuwa wameendelea kutumia teknolojia mbadala ya ujenzi wa madaraja ya mawe ambayo ni gharama nafuu kulinganisha na madaraja ya zege ili kuwaunganisha wananchi katika maeneo ya vijijini katika shughuli zao za biashara na huduma za kijamii na kiutawala.
Alisema wamejenga madaraja 19 ya mawe likiwemo daraja la mto Mwali pamoja na barabara zake ambalo limegharimu shilingi milioni 283 ujenzi wa madaraja haya yamekuwa ni mkombozi mkubwa sana kwa wananchi kwani wanafikia huduma za kijamii kwa urahisi.
Vilevile, alieleza kuwa TARURA mkoa wa Katavi imetekeleza miradi ya kimkakati inayogusa wananchi moja kwa moja, katika Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele wamejenga daraja la mto Msadya lenye urefu wa mita 60 kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.2 ili kurejesha mawasiliano ya wananchi wa kata za Mwamapuli, Chamalendi, Ikuba, Kibaoni na Majimoto.
Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Mwamapuli B wilayani Mpimbwe, Bw. Zengo Fareji, ameishukuru serikali kwa kujenga la Msadya ambalo limewasaidia kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.
Kwa upande wake, Bw. Nkolingo Selemani mkazi wa kijiji cha Majalila wilayani Tanganyika, ameishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja la mto Mwali ambalo linaunganisha vijiji vya Nyagantambo, Ifinsi na Bugwe kwani limewasaidia kusafirisha mazao yao na kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi.