Michuano ya soka Tulia Trust kwa ushirikiano na Raphael Group imezinduliwa rasmi katika Uwanja wa Mawinji Uyole ya Kati Mgeni rasmi akiwa ni Simon Sanga mchezaji wa zamani wa soka.
Meneja wa Tulia Trust Jacqueline Boaz amesema michuano hiyo inadhaminiwa kwa mwaka wa nne mfululizo ambapo mwaka huu imedhaminiwa kwa shilingi milioni kumi na moja na laki nne elfu hamsini.
Boaz amesema lengo la Taasisi ni kukuza michezo na kutoa fursa ya ajira kwa vijana na jumla ya timu thelathini na nne zinashiriki michuano hiyo na kila timu imepatiwa seti ya jezi na mipira.
Awali Mwenyekiti wa Chama Cha mpira wa Miguu Jiji la Mbeya John Gondwe amesema michuano hiyo imekuwa ikiibua vipaji kwa vijana Jijini Mbeya.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya Sadiki Jumbe amemuomba Mgeni rasmi kuwa mdhamini wa Chama Cha Wanawake mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya.
Akijibu ombi la ulezi wa Chama Cha mpira wa Miguu Simon Sanga amekubali kuwa mlezi wa Chama hicho.
Sanga ameomba wadau kutovamia Viwanja vya michezo ili vijana wapate maeneo ya kucheza waweze kuepukana na vitendo viovu.
Hata hivyo ameomba kutilia mkazo zaidi soka la Wanawake ambalo halijapewa kipau mbele Mkoani Mbeya.
Katika kutia hamasa michuano hiyo Taasisi ya Tulia Trust itatoa zawadi kwa mfungaji bora, golikipa bora na timu yenye nidhamu.
Mshindi wa kwanza atapata kikombe na pesa shilingi milioni tano,mshindi wa pili shilingi milioni tatu,wa tatu shilingi milioni mbili na mshindi wa nne atapata shilingi milioni moja.
Golikipa bora atapata shilingi laki moja, mfungaji bora shilingi laki moja,timu yenye nidhamu itapata shilingi laki moja mfungaji na kikundi chenye hamasa kitajinyakulia pia shilingi laki moja na mwandishi bora wa michezo atajinyakulia shilingi elfu hamsini.