UMWAGAJI ZEGE UJENZI WA BANIO MRADI MTO KIWIRA WAANZA
Miradi wa Maji mto Kiwira unaendelea kwa ufanisi mkubwa kama ilivyokusudiwa na kasi ikielekezwa kwenye umwagaji wa zege kwenye banio utakaodumu kwa saa thelathini na sita unaofanywa na kampuni ya China Railway Construction Group ambapo awali ilifanyika kazi ya kuchepusha mto.
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Barnabas Konga Mkurugenzi wa masuala ya Ufundi Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mbeya (MBEYAUWSA) ambaye pia ni Msimamizi wa mradi wa Maji mto Kiwira.
Konga amesema shughuli ya zege itafanyika usiku na mchana ili ifikapo mwezi machi mwakani mradi uwe umekamilika.
Aidha Konga amempongeza Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson kwa ufuatiliaji wa pesa za mradi sanjari na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa za utekelezaji wa mradi.
Konga amesema vijiji vya Unyamwanga, Mbeya 1 na Swaya vinavyopitiwa na mradi huo vitanufaika na huduma ya maji.
Robert Mkasela kutoka kampuni ya GKW anayemsimamia mkandarasi amesema mradi unasimamiwa kwa ubora, usalama na wakati uliokusudiwa.
Kwa upande wake Wang Yang mkandarasi wa mradi huo amesema mradi utakamilika kama ilivyokusudiwa lengo ni kukamilisha banio na tanki la kupokelea maji kabla ya msimu wa mvua kuanza.