Halmashauri ya Jiji la Mbeya imezitaka kampuni ya ujenzi ya Cico inayojenga jengo na barabara za mradi wa Tactic na Kampuni ya Mhandisi ambayo ni mkandarasi mshauri kwenye miradi hiyo kuwaondoa wasimamizi wake kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza baada ya ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za Kalobe-Itende, Machinjioni- Mapelele, Kabwe-Sido na Iziwa, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mhe.Dormohamed Issa amesema, hajaridhishwa na anapata wasiwasi na kasi ya maendeleo ya mradi na hana uhakika kama mkandarasi atamaliza mradi kwa wakati uliopangwa kwa mujibu wa mkataba.
Mstahiki Meya ameongeza kuwa tangu mkandarasi wa kampuni ya Cico alipokabidhiwa na kuanza kazi Novemba, 2023 hakuna alichokifanya kwenye barabara zote, hali ambayo inasababisha wananchi kuendelea kukabiliwa na changamoto ya barabara wakati Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, imeshatoa fedha, hivyo amemtaka mkandarasi kumuondoa Meneja Mradi Mhandisi Bw.Penfeng Wang na Kampuni ya Mhandisi ambayo ni Mkandarasi Mshauri, Bw.Jofrey Kanjanja kwa kushindwa kusimamia kasi ya mradi kama ilivyopangwa.
“Mkandarasi mshauri urafiki wako na Mkandarasi unatia wasiwasi, kazi haiendi haiwezekani kila wakati mko pamoja, hapo kazi haiwezi kwenda utashindwa kusimamia vyema mradi huu, naomba kampuni zenu zitubadilishie wasimamizi haiwezekani hata kidogo”, amesema Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya.
Katika hatua nyingine Mstahiki Meya amemtaka Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Bw.Leonard Mohosea kuhakikisha kila jumatatu anawasilisha taarifa za mwenendo wa mradi na kumsimamia ipavyo mkandarasi ili kufikia malengo ya mradi ambayo Serikali imejiwekea sambamba na kuwaondelea kadhia wananchini na kusiimua shughuli za maendeleo zitakazokuwa zikifanywa kupitia barabara hizo.
Mradi huo unaogharimu Shilingi Bilioni Ishirini na Moja(Bilioni 21) ukijumuisha barabara tano yenye urefu wa kilometa 12.3(km12.3) mifereji ya maji ya mvua yenye jumla ya urefu wa kilometa 6.4(km6.4) na ujenzi wa jengo la maabara ya udhibiti ubora, ulioanza Novemba, 2023 unatarajiwa kumamilika ifikapo Februari 2025.
Kesho Mei 23 2024 Mstahiki Meya anatarajia kuendelea na ziara kukagua utekelezaji wa miradi ya Tactic.