Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.
Timu maalumu ya kupambana na makosa ya mtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano TCRA wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 20 wakiwemo raia 04 wa Nchi jirani kwa makosa ya kuingilia mifumo ya mawasiliano.
Akitoa taarifa hiyo leo Oktoba 29, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti Mkoani Arusha kwa mwezi huu wa Oktoba 2024.
SACP Masejo amebainisha kuwa watuhumiwa 16 kati ya waliokamatwa ni mawakala wa kusajili laini za mitandao ya simu ambao wanasajili laini za simu kwa kutumia vitambulisho vya Taifa NIDA vya watu wengine bila ridhaa zao na kisha kuuza kwa wahalifu hao ambao huzitumia kuingilia mifumo ya mawasiliano na kufanya uhalifu.
Aidha katika ufuatiliaji walibaini kuwa laini nyingi wameziuza kwa raia hao 04 wa Nchi Jirani ambao walikutwa na mitambo ya mawasiliano aina ya Simbox, Laini mbalimbali za mitandao ya simu, kompyuta mpakato, komptyuta, simu za mikononi, invetor solar na betri za solar.
Kamanda Masejo amesema upelelezi wa shauri hilo umekamilika, na taratibu nyingine za kisheria zinafuata.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linatoa wito kwa watu wanaosajili laini za simu ambao sio waaminifu wanaotumia vitambulisho vya Taifa vya watu wengine kusajili laini na kuuza kwa watu wengine kuacha mara moja kwani wataendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.
Halikadhalika limetoa rai kwa wamiliki wa nyumba kuwa makini na wapangaji wanaowapangisha katika nyumba zao, kwani baadhi ya wahalifu hutumia nyumba hizo kufanya vitendo vya kihalifu.
Sambamba na hilo Jeshi la Polisi Mkoani humo limewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kila mara wa kupiga namba *106# ili kujua namba zilizosajiliwa kupitia vitambulisho vyao vya NIDA ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.